Na: Amina Hezron – Njombe.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu
cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Upande wa Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu
Prof. Maulid Walad Mwatawala amepongeza Watafiti wa Mradi wa GRILI kwa
kufanikiwa kufikia malengo yote matatu ya utafiti huo muhimu kwa Taifa.
Pongezi hizo amezitoa wakati
akifungua Mkutano Mkuu wa mwisho wa Mradi huo unaofanyika mkoani Njombe na kuwakutanisha
wadau wote wa mradi kutoka ndani na nje ya nchi kupokea matokeo ya mwisho ya
Mradi kutoka kwa wasimamizi wa Mradi huo na Wanafunzi waliokuwa wanasomeshwa na
mradi wakifanya tafiti mbalimbali.
“Sisi kama Chuo tumefurahishwa na
utekelezaji wa mradi huu ambao ulikuwa na malengo makuu matatu ya kujenga uwezo
na tutaona hapa waliyoyafanya, Kuzalisha elimu mpya pamoja na mifumo mipya ya biashara
kwenye eneo la mimea dawa ambayo ni muhimu kwa uchumi wa wadau kwenye mnyororo
wa thamani wa mimea dawa nchini” alisema Prof. Mwatawala.
Aidha amesema kama Chuo wamefarijika kuona mradi umezalisha Wanafunzi watano (5) wa Shahada ya uzamivu kwenye masuala ya Mimea dawa na saba (7) saba shahada ya uzamili ambao kwa ujumla wameweza kuzalisha machapisho ya kisayasi 17 kwenye eneo hilo muhimu huku akitumia nafasi hiyo kumpongeza Mkuu wa mradi huo Prof. Faith Mabiki kwa kazi kubwa aliyoifanya na wasimamizi wengine wa mradi huo ambao anaamini katika kipindi kifupi machapisho hayo ndiyo yamemuwezesha kupanda cheo kutoka Udaktari na kuwa Profesa.
Amesema mfumo mzuri wa biashara
ya bidhaa za mimea dawa uliotengenezwa na Mradi huo utakuwa kichocheo kizuri
cha mabadiliko na mafanikio ya biashara ya dawa asili kwakuwa anatambua dawa
hizo zinauzwa kila kona nchini na watu wanazitumia lakini sasa kwa mfumo huu
zitaweza kuuzwa katika mifumo rasmi.
“Kitu kingine muhimu ambacho ni
kizuri mradi huu umefanya ni kuwaunganisha wadau wote kwenye mnyororo wa thamani
wa bidhaa za mimea dawa kupitia Jukwaa lake la Ubunifu wa bidhaa zitokanazo na
mimea dawa (GRIP) ambalo limesaidia kuwaweka pamoja wadau wote na kujadiliana
maendeleo na changamoto na kuzitatua kwa pamoja ambalo linasimamiwa na SUA
lakini wazo lilitoka kwenye mradi huu wa GRILI” alipongeza Prof. Mwatawala.
Akizungumza malengo na mafanikio ya
Utafiti Mkuu wa Mradi huo Prof. Faith Mabiki amesema mradi ulijikita katika kushughulika
na bidhaa zitokanazo na mimea dawa kwa maana ya tiba asili na mnyororo mzima wa
thamani ili kusaidia Tanzania kunufaika na utajiri mkubwa ilionao wa maliasili
hususani mimea dawa kwa kufikia soko la
Dunia.
Mtafiti Mkuu wa Mradi wa GRILI Prof. Faith Mabiki akiwasilisha malengo na mafanikio ya Mradi huo. |
Aidha amesema utafiti huo
ulilenga kusaidia Tanzania kufikia mpango wake wa maendeleo wa 2025 unaotambua
mchango wa matumizi ya maliasili ikiweo mimea dawa ambayo ipo nchini na
inatumiwa lakini haijaweza kushika vyema soko la ndani na kimataifa na
kuchangia maendeleo ya wadau wa tiba asili.
Amesema changamoto kubwa
iliyoletwa na Tafiti zinazofanywa na mradi huo ni namna ambavyo sasa wanaweza
wakachukua matokeo ya mradi huo ili kuyakuza kuleta maendeleo ya wadau binafsi
katika kuongeza ubora na Masoko.
Prof. Mabiki amesema jambo lingine kubwa
ambalo kama Chuo wanajivunia na kufanikiwa kupata kifaa cha kisasa cha kupima
kemikali za mimea dawa, Madawa na vyakula ambacho kitaendeea kusaidia Watafiti,
Wanafunzi na wadau wengine kukikutumia katika kufanya tafiti mbalimbali hapahapa
nchini.
Mradi wa GRILI-DANIDA unatekelezwa
na Chuo Kikuu cha Sokoine(SUA) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Afya na
Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Chuo Kikuu cha Sayansi na teknolojia
Afrika cha Nelson Mandela (NM-AIST), Chuo Kikuu cha Mzumbe, Shirika la Utafiti
wa Maendeleo ya Viwanda Tanzania(TIRDO), Taasisi ya taifa ya Utafiti wa
magonjwa ya Binadamu, NIMR, Chuo kikuu cha Copenhagen cha nchini Denmark kwa
ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Denmark DANIDA.
PICHA ZA WASHIRIKI WA MRADI HUO WAKIFUATILIA MAWASILISHO
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma Prof. Lughano Jeremy Kusiluka akitambulisha washiriki na ratiba ya siku hiyo ya kwanza ya mkutano huo. |
Picha ya pamoja ya Washirika wa Mradi Mkutano huo kutoka taasisi mbalimbali nchini na kutoka nje ya Tanzania. |
0 Comments