SUAMEDIA

Serikali inahitaji sera kurasimisha biashara ya bidhaa za mimea dawa.

 Na­: Amina Hezron - Njombe

Watafiti wa Mradi wa GRILI uliohusisha uvumbuzi na utengenezaji wa mwongozo wa kibiashara wa bidhaa za mimea dawa wametakiwa kuwasilisha mapendekezo ya kisera ya utafiti huo Serikalini ili biashara hiyo iingie katika mfumo rasmi na hivyo kuchangia pato la Jamii na Taifa.

1.      Katibu Tawala Mkoa wa Njombe Bi. Judica Omary ambae alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa Mhe. Antony Mtaka katika Kongamano la kisera la wadau wa mnyororo wa thamani wa mimea dawa akifungua Kongamano hilo.

Hayo yamezungumzwa na Katibu Tawala Mkoa wa Njombe Bi. Judica Omary ambae alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa Mhe. Antony Mtaka katika Kongamano la kisera la wadau wa mnyororo wa thamani wa mimea dawa lililofanyika mkoani Njombe.

 “Ukamilifu na utekelezaji wa Ajenda 2030 hasa katika nchi zinazoendelea unategemea sana uwekezaji katika tafiti za kisayansi, Teknolojia, Ubunifu na Uvumbuzi kwa kuzingatia mahitaji yetu kwa uhalisia wake”, alisema Judica.

Aidha ameeleza kuwa Serikali imeazimia na kujitolea kuwezesha mtafiti mmoja mmoja na Taasisi mbalimbali kutafiti, kubuni, na kuboresha teknolojia katika sekta zote za kiuchumi ikiwemo sekta ya Viwanda ambayo kwa sasa inakua kwa kasi kubwa hivyo ametoa rai kwa watafiti kuendelea kufanya tafiti ambazo zitaibua ubunifu katika maendeleo ya sekta mbalimbali.

Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua kongamano hilo Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Upande wa Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Maulid Walad Mwatawala amesema zaidi ya asilimia 80 ya watanzania wanatumia dawa za asili zitokanazo na mimea kwa ajili ya afya na kujikimu kwa kipato.

“Zaidi ya yote, wadau wengine tayari wanasafirisha nje ya nchi mazao au sehemu za mimea hiyo kama biashara na kujipatia kipato na kuimarisha uchumi wao , soko la kimataifa la bidhaa za rasilimali za kijani (GRPs), ikiwa ni pamoja na dawa za asili, ni zaidi ya Dola za kimarekani bilioni 170 na linaendelea kukua kwa asilimia 15 kwa mwaka, huku kukiwa na shauku kubwa ya bidhaa mpya kutoka Afrika”, alisema Prof Mwatawala.

Akizungumzia yaliyofanyika kupitia mradi huo Mkuu wa Mradi kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Faith Mabiki amesema kuwa utafiti huo umeweza kutambulisha mnyororo wa thamani na kugundua wadau muhimu ambao wakishirikiana wanaweza kusaidia kuinua sekta ya mazao ya kijani hasa tiba asili kwenda kuchangia katika pato la Taifa na mtu mmoja mmoja.

“Kwahiyo wadau waliopo hapa wengi wanajiona katika mnyororo wa thamani huu na huu tumeutengenezea chapisho maalumu ambalo limetoka katika ulimwengu lakini pia tumeweza kutengeneza muundo wa kibiashara”, alisema Prof Mabiki.

Akitoa neno la shukrani kwa mgeni rasmi Mkurugenzi,Kurugenzi ya Shahada za Uzamili,Utafiti na Uhaulishaji wa Teknolojia kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Esron Karimuribo amesema kuwa anashukuru kwa ahadi za Serikali katika kuendelea kutumia matokeo ya tafiti ambazo zinasaidia katika kuandaa au kuboresha sera lakini pia maendeleo ya Taifa.

“Tunafarijika sana kama watafiti tukiona tunafanya kazi ambayo inaweza ikathaminiwa katika kutoa mchango kwa taifa tunashukuru sana, lakini umetuahidi serikali itakuwa na watafiti bega kwa bega katika shughuri zetu ikiwa  ni pamoja na habari ya kuongeza fedha na bajeti ya utafiti, kwetu sisi tupo tayari kwasababu tuna ujuzi na rasilimali fedha inapopatikana tunakuahidi tutatoa mchango wetu katika kutoa majawabu ambayo yanalikabili taifa na jamii “, alisema Prof. Karimuribo.

1.      Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Upande wa Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Maulid Walad Mwatawala akitoa salamu za SUA kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua Kongamano hilo.


1. Mkurugenzi,Kurugenzi ya Shahada za Uzamili,Utafiti na Uhaulishaji wa Teknolojia kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Esron Karimuribo akitoa neon la shukrani kwa mgeni rasmi.














Post a Comment

0 Comments