SUAMEDIA

Kampasi ya Mizengo Pinda (SUA) mkoani Katavi yasaidia kufikisha Elimu na Uelewa juu ya mazao mengine yatokanayo na Nyuki mbali na Asali

 Na: Tatyana Celestine , KATAVI

Imeelezwa kuwa kuwepo kwa Kampasi ya Mizengo Pinda mkoani Katavi ambayo ni Kampasi ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kumesaidia kuwafikia Wafugaji wa Nyuki ili kutoa elimu ya namna bora ya ufugaji wenye kuleta tija tofauti na ilivyokuwa awali kwani wakulima wengi wamekuwa wakifuga bila kuzingatia taratibu muhimu na kukosa uelewa juu ya mazao mengine yatokanayo na nyuki mbali na asali.


Akizungumza na SUAMEDIA mara baada ya kutembelea Chuoni hapo Mwanafunzi wa Shahada ya Nyuki na Usimamizi wa Rasilimali zake Bw. Naftari Josephat amesema kuwa yeye kusoma shahada hiyo ni kama fursa katika maisha yake kwani shahada hiyo inapatikana SUA pekee Tanzania.

Aidha amesema kuwa Shahada hiyo inampa mwanga mwanafunzi tangu anapoanza mwaka wa kwanza wa masomo kwa kushiriki katika mafunzo kwa vitengo kitu ambacho kinamuimarisha na kujiamini kuwa mara baada ya kuhitimu atakuwa na uwezo wa kujiingizia kipato yeye pamoja na Taifa kwa ujumla.

Bw. Josephat amewaasa vijana ambao wapo Sekondari kufikiria kujiunga kusoma kozi hiyo kwani inahitaji watu wengi na kwakuwa inapatikana SUA pekee basi ichukuliwe kama fursa kwao hivyo wale wenye vigezo ni nafasi yao kuweza kujiunga na Chuo.  

Nae Mwanafunzi wa Mwaka wa Pili kutoka Kampasi ya Mizengo Pinda Katavi Zubeda Nkama ameelezea umuhimu wa kujifunza Shahada hiyo kwa wasichana na kusema kuwa kusoma shahada hiyo ni faida kwa kuwa wanafunzi wanajifunza kwa vitendo moja kwa moja kama vile kutengeneza Mizinga, kujua idadi ya nyuki wanaokuwa kwenye mzinga, na kujua mazao mengine yatokanayo na nyuki tofauti na asali.

KATIKA VIDEO

Post a Comment

0 Comments