SUAMEDIA

SUA yaanza utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mabadiliko ya Kiuchumi (HEET) kupitia Kampasi ya Mizengo Pinda Katavi

 Na: Tatyana Celestine ,  Katavi        

Katika kutekeleza Mradi wa HEET, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Kampasi ya Mizengo Pinda iliyopo Katavi kimefanya Tathmini ya Mazingira na kijamii hususani kwenye suala la uboreshaji wa Elimu, kuongeza Miundombinu na kuanza kutekeleza Mradi huo ili kusaidia ongezeko la Wanafunzi, mazingira kuwa bora na ubora wa elimu chuoni hapo.



Rasi wa Kampasi ya Mizengo Pinda (SUA) Katavi, Prof. Josiah Katani akionesha maeneo ambayo yanatakiwa kufanyika utekelezaji wa Mradi wa HEET unaotarajiwa kuanza chuoni hapo. 

Akizungumzia kuhusiana na Mradi huo Mtaalam wa masuala ya Kijamii katika Mradi huo Prof. David Mhando amesema kuwa Mradi huo umepanga kufanya mambo manne kwa kuanza na ujenzi wa Mabweni ya Wanafunzi Bwalo la Chakula, uandaaji wa Shamba Darasa pamoja na kujenga Jengo Mtambuka maalum kwa kujifunzia.

Aidha Prof. Mhando amesema kuwa katika Mradi huo wamezingatia watu ambao wana mahitaji maalum ili nao waweze kufaidika na Mradi huo kama maelekezo ya Benki ya Dunia yalivyoagiza ili nao waweze kupata nafasi ya kujiendeleza kielimu bila changamoto yoyote.

Nae Mtaalam wa Mazingira katika Mradi wa HEET Dr. Amina Hamad amesema kuwa kutokana na lengo la Mradi huo Kwa Vyuo Vikuu ndio sababu ya kutembelea maeneo ambayo Mradi utafanyika katika Kampasi ya Mizengo Pinda na wamebaini kuwa hakuna kitakachozuia Mradi huo kutekelezeka kwa kuwa muda wote wa Mradi tathmini zitafanyika kwa kila hatua.

Kwa upande wake Rasi wa Kampasi ya Mizengo Pinda Prof. Josiah Katani amesema kuwa kwa kufikiwa na Mradi wa HEET kutawaletea mabadiliko makubwa kutokana na shughuli za ujenzi zitakazofanyika kwani itapelekea ongezeko la Wanafunzi vilevile kufungua fursa za kibiashara ndani na nje ya Chuo.

Aidha Prof. Katani amebainisha kuwa asilimia kubwa ya Wafanyakazi wa Kampasi hiyo wamefaidika na Mradi huo kwa kwenda kusoma hivyo mategemeo ya ubora wa elimu ni mkubwa mara baada ya walimu hao kuhitimu na kurejea kazini.

Pia  Wanafunzi walioshiriki katika kutoa maoni yao kuhusiana na Mradi huo unaotekelezwa  Chuoni hapo wamesema kuwa Mradi wa HEET  utakuwa na faida kwao kwani mara baada ya kuongezeka kwa miundombinu hivyo Maisha yao yatabadilika na kuepukana na gharama za kupanga nje ya Chuo kwani gharama hizo ni kubwa ukilinganisha na gharama za hostel za ndani.

Faida nyingine waliyoizungumzia ni urahisi wa upatikanaji wa Chakula pamoja na kuwezesha kubadilisha kwa mtaala wa kimasomo kwa kuongeza vitu vya muhimu katika masomo au kupunguza vitu ambavyo ni changamoto kwa mwanafunzi itakayopelekea kupata elimu iliyo Bora na ya uhakika.

Rasi wa Kampasi ya Mizengo Pinda SUA Katavi Prof. Josiah Katani akizungumza na Mtaalam wa Mazingira pamoja  na Mtaalam wa masuala ya kijamii walipotembelea chuoni hapo. ( Wa kwanza kushoto ni Mtaalam wa Mazingira Dr. Amina Hamad, (katikati Mtaalam wa Masuala ya kijamii Prof. David Mhando).




Picha mjongeo  itakujia hivi punde...


 

Post a Comment

0 Comments