Na Gerald Lwomile
SUA
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimesema endapo
kutakuwa na matumizi endelevu ya Teknolojia ya Mawasiliano nchini yasiyo na
vikwazo basi Kilimo cha nchi hii kinaweza kukua kwa kasi na kuwa na tija kwa
mkulima binafsi na Taifa kwa ujumla.
Hayo yamesemwa na Prof. Wulystan Mtega kutoka SUA wakati
akitoa salaamu kwa niaba ya Mkuu wa Kampasi ya Solomon Mahlangu katika ufunguzi
wa Mhadhara wa siku mbili unaofanywa na Mradi wa ‘SUA YEESI Lab’ unaowawezesha
vijana kutumia akili bandia katika kuangalia changamoto mbalimbali katika
kilimo.
Prof. Mtega amesema hivi sasa namba ya Wataalamu ni ndogo
katika kuwafikia wakulima nchini hivyo utumiaji wa Teknolojia ya Mawasiliano
unaweza kuja na aina ya mawasiliano ‘App’ inayoweza kutatua changamoto mbalimbali
katika kilimo kwa upatikanaji wa taarifa sahihi na muhimu kwa wakati.
Naye Mkuu wa Mradi huo Dkt. Kadeghe Fue ambaye pia ni Mhadhiri
SUA amesema Mradi huo umelenga kuwajengea uwezo vijana katika kuhakikisha
wanakuwa na matumizi sahihi ya Teknolojia ya Mawasiliano na Habari na hasa
kwenye kilimo ili kutatua changamoto zinazowakabili wakulima.
http://suamedia1994.blogspot.com/2022/05/matumizi-ya-teknolojia-ya-mawasiliano.html
Dkt. Fue amesema katika kutumia teknolojia hiyo ya akili
bandia wanafunzi wanaweza kujifunza namna ya kuangalia changamoto katika kilimo
kama magonjwa, magugu, namna mmea unavyoendelea shambani kwa kutumia vifaa kama
Kompyuta, Kamera na vingine kama hivyo ili kuona tabia ya mmea katika makuzi
yake.
Amesema kutokana na utaalamu watakaoupata vijana hao wanaweza
kuanzisha Makampuni ambayo yatasaidia kuangalia na kupata taarifa sahihi zitakazosaidia
kutatua changamoto lakini pia kuwa kichocheo cha mabadiliko katika namna ya
kufanya kilimo chenye tija.
Amesema kuwa matumizi ya Teknolojia hizi yamerahisishwa kiasi
mkulima anaweza kupiga picha au kutuma sauti kwa njia ya mtandao na kupata suluhisho
la changamoto ya ugonjwa au kutokuwepo kwa maendeleo katika mmea wake.
Naye Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Georgia cha nchini
Marekani Prof. Glen Rains amesema kuwa tangu kumalizika kwa vita kuu ya pili ya
Dunia mwaka 1945, Dunia ikiwemo Marekani iliingia katika changamoto kubwa ya
uharibifu wa mazingira na ndipo teknolojia za kisasa zikaanza kutumika ili
kuhakikisha uzalishaji wa mazao ya kilimo unaongezeka.
Washiriki wa Mradi wa SUA YEESI Lab wakisikiliza mawasilisho kutoka kwa Prof. Rains
Amesema ni muhimu wakulima wakatumia teknolojia za kisasa
ikiwemo Teknolojia ya Mawasiliana na Habari katika kuhakikisha wanatatua
changamoto mbalimbali katika sekta hiyo muhimu ili kuongeza uzalishaji wa mazao
ya kilimo.
Ametolea mfano kuwa uzalishaji wa mazao ya Pamba umeongezeka
maradufu kufuatia kuwepo kwa Teknolojia hizo za Mawasiliano kama mtandao na kwa kutumia vifaa kama Mkongo,
Kompyuta na Kamera changamoto nyingi zimetatuliwa na kuinua kilimo kwa kiasi
kikubwa
0 Comments