Na Farida Mkongwe, Dar es Salaam
Wakulima nchini wametakiwa kufuata kanuni na taratibu bora za
kilimo ikiwa ni pamoja na kujua afya za mashamba yao kabla ya kuanza kulima ili
waweze kupata mavuno yenye tija.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza kwa wingi katika banda la SUA wakipata maelezo na kufanya udahili wa kujiunga na chuo hicho kwenye maonesho ya Vyuo Vikuu (TCU) jijini Dar es Salaam
Ushauri huo umetolewa na Mtaalamu wa Maabara ya Udongo kutoka
Ndaki ya Kilimo, Idara ya Sayansi ya Udongo na Jiolojia wa Chuo Kikuu cha
Sokoine cha Kilimo SUA Bw. Stevenson Pelegy Noah wakati akizungumza na SUAMEDIA
katika Maonesho ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayofanyika jijini Dar
Es Salaam.
Bw. Noah amesema ili kujua afya ya shamba mkulima anatakiwa
apime udongo na kujua virutubisho vilivyomo kwenye udongo vinafaa kwa mazao ya
aina gani, kujua aina ya mbolea inayohitajika pamoja na kupata ushauri kutoka
kwa wataalamu ili aweze kufikia malengo yake.
“Hapa tumekuja na maabara ya udongo inayobebeka, kazi yake
kubwa ni kupima virutubisho vya mimea vilivyopo kwenye udongo, kwa hiyo mtu
akija na sampuli ya udongo kutoka shambani kwake kama katumia vile vigezo
tunavyohitaji basi tutampimia na kumpa ushauri bure”, alisema Bw. Noah.
Amesema kwa wakulima ambao watashindwa kupima udongo wanaweza
kugundua mapungufu yaliyopo kwenye udongo uliopo kwenye mashamba yao kwa kuangalia
rangi na aina ya udongo uliopo shambani kwake na pia anaweza kutumia dalili
mbalimbali ambazo zinajitokeza kwenye mimea inayoota mashambani.
Amezitaja baadhi ya dalili hizo kuwa ni mmea kudumaa na kuwa
na rangi ya njano, majani ya mwanzo kukauka mapema, mmea kuwa na rangi ya
zambarau na mimea kuwa na michirizi ya njano ambapo amesema hizo ni dalili za
mimea kuwa na mapungufu ya nitrojeni, fosforas, salfa au potassium ambapo
mkulima anatakiwa kupata ushauri kutoka kwa wataalamu ili ajue namna ya
kukabiliana na mapungufu hayo.
0 Comments