SUAMEDIA

Waziri Kapinga atembelea banda la SUA na kuona teknolojia mbalimbali za kilimo

 Na: Farida Mkongwe

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, ametembelea banda la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) katika Maonesho ya Nanenane yaliyoanza Agosti 1, 2026, na kujionea teknolojia mbalimbali za kisasa zinazolenga kuimarisha uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.


Akiwa katika banda hilo, Mhe. Kapinga alitembelea maeneo mbalimbali ya maonesho na kupata maelezo kuhusu teknolojia na ubunifu unaofanywa na watafiti wa SUA kwa ajili ya kuwasaidia wakulima, wafugaji na wavuvi kuongeza tija, kuboresha uzalishaji na kuongeza thamani ya bidhaa zao.

Waziri Kapinga alipokelewa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Amandus Muhairwa, kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Raphael Chibunda.

Katika ziara hiyo, Mhe. Kapinga alijionea teknolojia zinazohusu uzalishaji wa mazao, ufugaji wa kisasa, uvuvi na uchakataji wa mazao, pamoja na bidhaa mbalimbali za kibunifu zinazotokana na tafiti zinazofanywa na chuo hicho. Aidha, alipata maelezo kutoka kwa wataalamu na watafiti kuhusu matumizi na manufaa ya teknolojia hizo kwa wazalishaji na jamii kwa ujumla.

Ushiriki wa SUA katika Maonesho ya Nanenane unaendelea kuwa jukwaa muhimu la kuunganisha tafiti, teknolojia na matumizi yake katika mazingira halisi ambapo kupitia maonesho hayo, chuo kinatoa elimu, ushauri wa kitaalamu na teknolojia kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wadau wengine, kwa lengo la kuongeza tija na kuchangia maendeleo endelevu ya sekta ya kilimo nchini.





Post a Comment

0 Comments