Na: Ngolo Mboje
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeendelea kuonesha
ubunifu katika Maonesho ya Nanenane 2026 kwa kuwasilisha teknolojia mbalimbali
za ushonaji na utengenezaji wa bidhaa zinazotokana na malighafi za asili,
ikiwemo teknolojia ya kuzalisha nyuzi kutoka kwenye majani ya nanasi.
Akizungumza katika maonesho hayo, Mhadhiri wa SUA kutoka Idara ya Lishe na Stadi za Mlaji, Dkt. Zahara Majili, amesema miongoni mwa ubunifu uliowasilishwa mwaka huu ni teknolojia ya kuzalisha nyuzi kutoka kwenye majani ya nanasi, ambazo hutumika kutengeneza bidhaa mbalimbali.
Amesema nyuzi hizo zinaweza kutumika kutengeneza mikoba,
mikanda, mapambo ya mezani pamoja na bidhaa nyingine za matumizi ya nyumbani,
hatua inayosaidia kuongeza thamani ya mabaki ya mimea ambayo mara nyingi
hutupwa baada ya kuvuna matunda ya nanasi.
Dkt. Zahara amesema SUA pia inaonesha teknolojia ya
kutengeneza rangi za asili zinazozalishwa kutoka kwenye mimea, ikiwemo manjano.
Rangi hizo hutumika kutengeneza vitambaa vya batiki kwa njia rafiki kwa
mazingira na salama kwa watengenezaji na watumiaji.
Aidha, amesema katika banda hilo kuna bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa kwa kutumia ngozi kwa ajili ya urembo, mavazi na mapambo ya ndani ambapo wananchi wanaotembelea banda hilo wanapatiwa elimu kuhusu namna ya kutengeneza bidhaa hizo pamoja na fursa za ajira na biashara zinazopatikana katika sekta za ngozi, ushonaji na ubunifu wa mavazi.
Dkt. Zahara amewahimiza wanafunzi kutembelea mabanda ya SUA
katika maonesho hayo kwa kuwa teknolojia na shughuli zinazooneshwa ni sehemu
muhimu ya mafunzo yao kwa vitendo, yanayowaandaa kuajiriwa au kujiajiri baada
ya kuhitimu masomo.
Pia, amewakaribisha wananchi kutembelea mabanda ya SUA,
hususan eneo la ushonaji na ubunifu wa mavazi, ili kujifunza teknolojia za
kisasa za ushonaji, utengenezaji wa bidhaa za ngozi na matumizi ya malighafi za
asili katika kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini.


0 Comments