Na: Calvin Gwabara – Dar es salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa wa Mamlaka ya
Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA) CPA Habibu Suluo ameipongeza Serikali kwa
uamuzi wa kuanzisha Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria ili kuongeza ufanisi
katika utekelezaji wa majukumu makubwa na nyeti
ya Ofisi hiyo nchini.
Ameyasema hayo wakati akizungumza
na Menejimenti ya Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria walipotembelea LATRA
kujifunza namna ofisi hiyo inavyotumia mifumo mbalimbali ya kielekitroniki
katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku wakati wakijiandaa kuanzisha
mifumo kwenye Ofisi hiyo mpya ya OCPD.
“Sisi kama LATRA tunatambua
umuhimu na unyeti wa Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria na mmekuwa na mchango
mkubwa sana katika utekelezaji wa majukumu yetu, tunawapongeza kwa kuwa Ofisi
kamili na tunawahidi ushirikiano wa hali na mali ili muweze kupata kile
mnachohitaji kujifunza kutoka kwetu” Alisema CPA Suluo.
Kwa upande wake Kaimu Mwandishi Mkuu wa Sheria ambaye ameongoza menejimenti ya
OCPD, Bi. Rehema Katuga ameeleza historia ya uanzishwaji wa Ofisi hiyo pamoja
na majukumu yake makuu ya Uandishi wa Sheria, Urekebu pamoja na Ufasili wa
sheria.
Bi. Katuga ameishukuru Serikali kwa kufanya uwekezaji mkubwa katika kuimarisha
Ofisi hiyo ikiwemo rasilimali watu, fedha na vitendea kazi ili kuweza
kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwa maendeleo ya taifa.
“Katika kipindi kifupi tumeweza
kupata mafanikio makubwa ikiwemo kufanikiwa kufanya Ufasili wa sheria kuu 446
Kwa lugha mbili yaani Kiswahili na Kiingereza ili kuwezesha watanzania wa
kawaida kuweza kusoma sheria na kuzielewa vizuri lakini pia wawekezaji kuzipata
kwa lugha ya kiingereza na toleo hilo litatoka hivi karibuni” alisema Bi.
Katuga.
Aliongeza “Pia tulifanikiwa kutoa
Toleo la Sheria zilizofanyiwa Urekebu la Mwaka 2023 na sasa tunatoa toleo la
urekebu la nyongeza kila mwaka ili sheria zinapofanyiwa marekebisho zisomeke
vizuri na hivyo kuwapatia watumiaji sheria zinazoenda na wakati badala ya kuwa
na vipande vipande ndani ya miaka kumi ambavyo vinafanya zoezi la rejea kuwa
gumu kwa watumiaji”.
Aidha amesema ziara hiyo ya
mafunzo ina lengo la kuhakikisha Ofisi yao inafikia lengo la matumizi ya
karatasi kuwa chini ya asilimia 10 katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya
kiofisi na hivyo kazi zote kufanyika kupitia mifumo ya kielekitroniki na kwa
haraka.
“Kutoka na uzito wa majukumu yetu
mara nyingi tunakuwa tumetawanyika sana hivyo tunataka popote mtumishi
atakapokuwa aweze kutekeleza majukumu ya kiofisi badala ya kulazimika kuwa
Ofisini kutumia karatasi na hii itasaidia kuongeza ufanisi na tija kwa ofisi
yetu na ndio maana tunataka kutumia mifumo imara na mizuri” alifafanua Bi.
Katuga.
Katika ziara hii ya mafunzo, menejimenti ya OCPD pia ilitembelea Ofisi ya
Wakili Mkuu wa Serikali (OSG) pamoja na Bohari Kuu ya Dawa (MSD).
| Menejimenti ya Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria na LATRA wakiwa kwenye picha ya pamoja mara bada ya kuhitimishwa kwa ziara hiyo. MATUKIO KATIKA PICHA WAKATI WA MAJADILIANO NA KUBADILISHANA UZOEFU |
0 Comments