Na: Ngolo Mboje
Watumishi
wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wamepatiwa mafunzo maalum ya kuwajengea
uwezo katika kudhibiti vihatarishi vinavyoweza kuathiri utendaji wa taasisi,
kufuatia mwongozo wa Serikali wa mwaka 2023 kuhusu usimamizi wa vihatarishi
katika taasisi za umma.
Mafunzo hayo yametolewa tarehe 21 Novemba, 2025 katika Kampasi ya Edward Moringe mjini Morogoro, yakilenga kuongeza uelewa, umahiri na uwezo wa watumishi katika kutambua, kuchambua na kudhibiti vihatarishi kwenye idara zao.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mwezeshaji kutoka Wizara ya
Fedha, Bw. Bariki Mtunha, amesema Serikali imeweka msisitizo
kwa taasisi za umma kuimarisha mifumo ya udhibiti wa vihatarishi ili kuboresha
uwajibikaji na ufanisi wa taasisi.
Amesema mafunzo hayo yameandaliwa kwa lengo la kuwasaidia watumishi wa SUA kupata uelewa mpana juu ya namna ya kusimamia masuala ya vihatarishi kwa ufanisi zaidi.
Mtunha ameongeza kuwa SUA imeonesha mafanikio makubwa katika kuimarisha mifumo hiyo na akawataka washiriki kuhakikisha elimu waliyoipata inasambazwa kwa watumishi wengine katika idara mbalimbali za chuo.
Kwa upande wake, Mratibu wa Vihatarishi wa SUA, Dkt. Coletha Mathew,
amesema mafunzo hayo yamewajengea uwezo mkubwa machampioni
watakaokuwa mstari wa mbele kusaidia shughuli za udhibiti wa vihatarishi chuoni.
Amesema kuwa mafunzo hayo ni endelevu na yatachangia kupunguza changamoto
zinazoathiri utendaji wa chuo, huku akitoa wito kwa Menejimenti ya SUA
kutekeleza kikamilifu miongozo ya Serikali ili kulinda utekelezaji wa malengo
ya taasisi.
Naye Mhadhiri kutoka Ndaki ya Uchumi na Stadi za Biashara (COEBS), Dkt. Hamad Ghaiza, aliyeshiriki mafunzo hayo, amesema yamewasaidia kuelewa kwa undani namna ya kutambua na kudhibiti vihatarishi vinavyoikabili taasisi.
Ameeleza
kuwa ujuzi huo utaiwezesha SUA kuboresha mikakati na mifumo ya utendaji,
sambamba na kufanikisha malengo ya mipango mkakati ya chuo.
Mafunzo haya yanatarajiwa kuimarisha usimamizi
wa vihatarishi katika idara zote za SUA na kuongeza ufanisi katika utekelezaji
wa majukumu ya chuo kwa ujumla.

0 Comments