SUAMEDIA

Prof. Kinabo afunga Mkutano wa ANH2025 kuomba watafiti na wadau kushirikiana kutatua changamoto za jamii

 Na: Calvin Gwabara - Dara ess salaam

Mwenyeji mwenza wa mkutano huo, Prof. Joyce Kinabo kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), ametoa wito wa kuendeleza ushirikiano, utekelezaji wa sera zinazotegemea ushahidi wa kisayansi, na ubunifu wa kisekta ili kukabiliana na changamoto za kimataifa katika mifumo ya chakula na afya ya umma.

Mwenyeji mwenza wa mkutano huo, Prof. Joyce Kinabo kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) akito hotuba ya kufunga Mkutano huo wa kimataifa jijini Dar es salaam.

Prof. Kinabo amesema hayo wakati akitoa hotuba yake ya kufunga mkutano huo wa kimataifa wa Kilimo Lishe na Afya (ANH2025) uliofanyika jijini Dar es Salaam, Tanzania na kuwakutanisha wataalamu wabobevu kwenye sekta hizo duniani zaidi ya 1500 ambapo 450 walishiriki ukumbini hapo na zaidi ya 1000 walishiriki kwa njia ya mtandao.

Prof. Kinabo alishukuru Chuo Kikuu cha London cha Usafi wa Mazingira na Tiba ya Kitropiki (LSHTM) kwa kuchagua Tanzania na Chuo Kikuu cha Sokoine kuwa wenyeji wa tukio hili kubwa la kimataifa na kueleza fursa hiyo kuwa ni heshima kubwa na ishara ya kutambua mchango wa Tanzania katika kuunda sera za kimataifa kuhusu chakula na afya.

“Tuendelee kutumia maarifa na uhusiano tulioupata hapa katika kazi zetu na ushirikiano wa baadaye,” Alisema Prof. Kinabo.

Aidha alieleza kwa muhtasari mambo muhimu yaliyoibuliwa katika mkutano huo, akisisitiza umuhimu wa mawasiliano baina ya sekta na taaluma mbalimbali, mshikamano kati ya utafiti na sera, na uhitaji wa kuwekeza zaidi katika mifumo ya maarifa hata hivyo alionya kuhusu hatari zinazoongezeka kama vile ulaji wa vyakula vilivyosindikwa kupita kiasi (UPFs), matumizi ya plastiki, na sumu katika chakula, ambavyo vinachukua nafasi ya lishe bora katika jamii nyingi.

Akitoa wito wa hatua za kuchukua alisisitiza kuwa changamoto tata zilizojadiliwa katika mkutano huu haziwezi kutatuliwa kwa njia za kisekta pekee bali aliwataka washiriki kutafsiri elimu waliyopata kuwa vitendo, kuendeleza ushirikiano baina ya mataifa na fani mbalimbali, na kuleta mabadiliko ya kimfumo.

 “Sasa na baadaye viko mikononi mwetu,” alisema Prof. Kinabo.

Prof. Kinabo pia alitoa shukrani kwa wawasilishaji wa mada, watafiti, washirika wa utekelezaji, na wafadhili waliofanikisha mkutano huo, na kumalizia kwa kuwataka washiriki kutazama mbele, akihimiza utafiti zaidi, uundaji wa vipimo vya pamoja vya kutathmini programu, na utekelezaji wa sera zinazotegemea ushahidi.

“Huu si mwisho, bali ni mwanzo wa fursa mpya na ushirikiano mpana zaidi,” alisema, kabla ya kutangaza rasmi kufungwa kwa mkutano wa kitaaluma wa ANH2025.

MATUKIO KATIKA PICHA KATIK SIKU YA MWISHO YA MKUTANO HUO


Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma Utafiti na ushauri wa Kitaalamu Prof. Maulid Mwatawala akizungumza kwenye kama mmoja wa wachokoza mada.

















Post a Comment

0 Comments