SUAMEDIA

SUA kupitia Mradi wa HEET waanza ujenzi wa majengo Katavi

 

Na: George Alexander

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) kimeanza ujenzi wa majengo katika Kampasi ya Mizengo Pinda ambapo Mkandarasi anafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati.



Akizungumza na SUA Media kwa niaba ya Mkuu wa Kampasi hiyo, Kaimu Mkuu wa Kampasi ya Mizengo Pinda Prof. Jeremiah Makindara ambaye pia ni Naibu Mkuu Mipango,Utawala na Fedha, amesema mradi huo wa miezi 18 uliotiwa saini mwishoni mwa mwaka 2024, unajumuisha ujenzi wa majengo mawili ambayo ni jengo litakalojumuisha madarasa, ofisi mbalimbali na kumbi na jengo la pili ni bweni lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 600 kwa wakati mmoja.

“Mkandarasi anaendelea na ujenzi wa majengo yote mawili licha ya kuchelewa kidogo kutoka kwa vibali vyao vya kufanya kazi nchini lakini anajitahidi kufidia muda wote uliopotea kwa kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha anamaliza kazi kwa wakati uliopangwa wakati wa utiaji wa saini”, amesema Prof. Makindara.

Ameongeza kuwa wanasimamia vyema ujenzi huo kwa kushirikiana na wahandisi wa Serikali waliopo eneo la ujenzi kwa lengo la kuhakikisha mkandarasi anatekeleza vyema majukumu yake na kuzingatia ubora uliowekwa.


Kwa upande wake Msimamizi wa Mradi upande wa Mwajiri Mhandisi  Hussein Mzimbiri amesema mpaka sasa mkandarasi ameweka msingi ambao utabeba nguzo zitakazoshikilia kuta za majengo hayo, huku akibainisha kasi ya mkandarasi ni nzuri na wao kama Serikali na washauri wataendelea kumsimamia mkandarasi huyo katika hatua zote za ujenzi zinazoendelea.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Mwanamvua Mrikondo amesema majengo hayo yataleta mageuzi makubwa katika mkoa wa Katavi ikiwemo ongezeko la udahili wa wanafunzi katikaKampasi hiyo na kuchochea ukuaji wa uchumi kwa kuwavutia wawekezaji mbalimbali.

“ Sisi kama Mkoa kwetu ni manufaa makubwa sana kwa sababu ongezeko la watu linakuja na manufaa mbalimbali kwa mfano ongezeko la ufanyaji wa biashara, mfano wanafunzi, wahadhiri na watumishi mbalimbali watakuwa wanahitaji chakula, malazi, usafiri, mafuta pamoja na huduma mbalimbali”, amesema Mhe. Mwanamvua.

Amesema kupitia upanuzi wa Chuo hicho wananchi wa Katavi wataweza kusoma kozi fupi fupi zitakazokuwa zinatolewa hapo ikiwemo kilimo, ufugaji wa nyuki na bila kuangalia umri wa mtu, ambapo tofauti na sasa ili kuweza kupata masomo hayo ya muda mfupi ni mpaka kusafiri hadi Morogoro.

Mhe. Mwanamvua amemuhakikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia suluhu Hassan kuwa pesa zote zilizolewa mkoani kwake kwa ajili ya ujenzi wa majengo hayo mawili yenye thamani ya shilingi Bilioni 17 wanazisimamia ipasavyo.

“Niliwaambia wana SUA na Wana Mpimbwe tangu siku tunasaini Mkataba kuwa mimi mwenyewe nahamia Mpimbwe, nahamia kwa maana ya kusimamia kwa karibu kila hatua ya usimamizi wa huu mradi wa bil 17  kuhakikisha pesa hizi tunazisimamia vizuri ili kujenga majengo yenye ubora wa Serikali”, ameongeza Mhe. Mwanamvua.

Mhandisi Li Kuan kwa niaba ya mkandarasi anayejenga majengo hayo ameihakikishia SUA Media kuwa ujenzi utaisha kwa muda uliowekwa licha ya kuwepo kwa baadhi ya changamoto ikiwepo upatikanaji wa vifaa vya ujenzi kuvitoa mbali lakini wanajitahidi usiku na mchana waweze kukamilisha kazi hiyo.

Amesema wamefurahia uhusiano mzuri uliopo kati yao na wanakijiji wa eneo wanapotekeleza mradi na kwamba hata Serikali inawapa ushirikiano mzuri katika ujenzi huo ambao kwa sasa umefikia asilimia 4.

Nao wanafunzi wanaosoma fani mbalimbali katika Kampasi hiyo wameishukuru Serikali kwa kuwezesha upatikanaji wa majengo hayo yanayofadhiliwa na HEET kuwa yatawawezesha kupata malazi yaliyo bora na kuwa karibu na madarasa na kuwahi vipindi hata nyakati za mvua.

Makubaliano ya Mradi huo wa majengo ya HEET unaofadhiliwa na Benki ya Dunia wenye thamani ya shilingi Bilioni 17 yalifanyika mwezi Novemba 2024, chini ya Kampuni ya ujenzi ya China ambayo imekusudia kukamilisha majengo mawili katika Kampasi ya Mizengo Pinda yatakaayowezesha kuongeza idadi ya wanafunzi katika udahili kutoka wanafunzi 200 kwa sasa mpaka wanafunzi 2,000.







 

Post a Comment

0 Comments