Na: George Alexander
Chuo Kikuu cha Sokoine cha
Kilimo (SUA) kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET)
kimeanza ujenzi wa majengo katika Kampasi ya Mizengo Pinda ambapo Mkandarasi
anafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa
wakati.
Akizungumza na SUA Media kwa niaba ya Mkuu wa Kampasi hiyo, Kaimu Mkuu wa Kampasi ya Mizengo Pinda Prof. Jeremiah Makindara ambaye pia ni Naibu Mkuu Mipango,Utawala na Fedha, amesema mradi huo wa miezi 18 uliotiwa saini mwishoni mwa mwaka 2024, unajumuisha ujenzi wa majengo mawili ambayo ni jengo litakalojumuisha madarasa, ofisi mbalimbali na kumbi na jengo la pili ni bweni lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 600 kwa wakati mmoja.
“Mkandarasi anaendelea na ujenzi wa majengo yote mawili licha ya kuchelewa kidogo kutoka kwa vibali vyao vya kufanya kazi nchini lakini anajitahidi kufidia muda wote uliopotea kwa kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha anamaliza kazi kwa wakati uliopangwa wakati wa utiaji wa saini”, amesema Prof. Makindara.
Ameongeza kuwa wanasimamia
vyema ujenzi huo kwa kushirikiana na wahandisi wa Serikali waliopo eneo la
ujenzi kwa lengo la kuhakikisha mkandarasi anatekeleza vyema majukumu yake na
kuzingatia ubora uliowekwa.
Kwa upande wake Msimamizi wa Mradi upande wa Mwajiri Mhandisi Hussein Mzimbiri amesema mpaka sasa mkandarasi ameweka msingi ambao utabeba nguzo zitakazoshikilia kuta za majengo hayo, huku akibainisha kasi ya mkandarasi ni nzuri na wao kama Serikali na washauri wataendelea kumsimamia mkandarasi huyo katika hatua zote za ujenzi zinazoendelea.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe.
Mwanamvua Mrikondo amesema majengo hayo yataleta mageuzi makubwa katika mkoa wa
Katavi ikiwemo ongezeko la udahili wa wanafunzi katikaKampasi hiyo na kuchochea
ukuaji wa uchumi kwa kuwavutia wawekezaji mbalimbali.
“ Sisi kama Mkoa kwetu ni
manufaa makubwa sana kwa sababu ongezeko la watu linakuja na manufaa mbalimbali
kwa mfano ongezeko la ufanyaji wa biashara, mfano wanafunzi, wahadhiri na
watumishi mbalimbali watakuwa wanahitaji chakula, malazi, usafiri, mafuta
pamoja na huduma mbalimbali”, amesema Mhe. Mwanamvua.
Amesema kupitia upanuzi wa Chuo
hicho wananchi wa Katavi wataweza kusoma kozi fupi fupi zitakazokuwa zinatolewa
hapo ikiwemo kilimo, ufugaji wa nyuki na bila kuangalia umri wa mtu, ambapo
tofauti na sasa ili kuweza kupata masomo hayo ya muda mfupi ni mpaka kusafiri
hadi Morogoro.
Mhe. Mwanamvua amemuhakikishia Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia suluhu Hassan kuwa pesa zote
zilizolewa mkoani kwake kwa ajili ya ujenzi wa majengo hayo mawili yenye
thamani ya shilingi Bilioni 17 wanazisimamia ipasavyo.
“Niliwaambia wana SUA na Wana
Mpimbwe tangu siku tunasaini Mkataba kuwa mimi mwenyewe nahamia Mpimbwe, nahamia
kwa maana ya kusimamia kwa karibu kila hatua ya usimamizi wa huu mradi wa bil
17 kuhakikisha pesa hizi tunazisimamia
vizuri ili kujenga majengo yenye ubora wa Serikali”, ameongeza Mhe. Mwanamvua.
Mhandisi Li Kuan kwa niaba ya mkandarasi anayejenga majengo hayo ameihakikishia SUA Media kuwa ujenzi utaisha kwa muda uliowekwa licha ya kuwepo kwa baadhi ya changamoto ikiwepo upatikanaji wa vifaa vya ujenzi kuvitoa mbali lakini wanajitahidi usiku na mchana waweze kukamilisha kazi hiyo.
Amesema wamefurahia uhusiano mzuri
uliopo kati yao na wanakijiji wa eneo wanapotekeleza mradi na kwamba hata Serikali
inawapa ushirikiano mzuri katika ujenzi huo ambao kwa sasa umefikia asilimia 4.
Nao wanafunzi wanaosoma fani
mbalimbali katika Kampasi hiyo wameishukuru Serikali kwa kuwezesha upatikanaji
wa majengo hayo yanayofadhiliwa na HEET kuwa yatawawezesha kupata malazi yaliyo
bora na kuwa karibu na madarasa na kuwahi vipindi hata nyakati za mvua.
Makubaliano ya Mradi huo wa majengo ya HEET unaofadhiliwa na Benki ya Dunia wenye thamani ya shilingi Bilioni 17 yalifanyika mwezi Novemba 2024, chini ya Kampuni ya ujenzi ya China ambayo imekusudia kukamilisha majengo mawili katika Kampasi ya Mizengo Pinda yatakaayowezesha kuongeza idadi ya wanafunzi katika udahili kutoka wanafunzi 200 kwa sasa mpaka wanafunzi 2,000.
0 Comments