SUAMEDIA

Ujenzi wa Mradi wa Bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere wakamilika kwa asilimia 99.8

Na: Gerald Lwomile 

Serikali imesema ujenzi wa Mradi wa Julius Nyerere Hydropower Project (JNHPP) wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115 ulioanza mwezi Juni 2019 umefikia asilimia 99.8 na mpaka sasa, jumla ya mashine 8 kati ya 9 zimeshawashwa na kufanya jumla ya Megawati 1,880 kuongezeka kwenye Gridi ya Taifa ya Umeme.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa akizungumza na waandishi wa habari 

Hayo yamesemwa tarehe 16 Februari, 2025 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa katika mkutano wake na vyombo vya habari uliofanyika katika Bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere, Rufiji mkoani Pwani.

Msigwa amesema mradi huu ambao uliachwa ukiwa na asilimia 33 tu na Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli umekuwa na maendeleo mazuri kwani Mhe. Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amehakikisha miradi yote iliyoachwa na mtangulizi wake inaendelea katika viwango vya hali ya juu.

Msemaji wa Serikali amesema tuta kuu ambalo hutumika kuhifadhi maji ya kuzungusha mashine kwa ajili ya kufua umeme ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 100 na lina Urefu wa mita 1,036; kina cha mita 131 na lipo kwenye eneo la kilomita za mraba 914 na lina uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo bilioni 32.8.

 

 Bwawa la JNHPP

Msigwa amesema mahandaki matatu ya kusafirisha maji kuelekea kwenye mitambo nayo yamekamilika kwa asilimia 100 na jengo la mitambo likiwa na mitambo tisa ya kuzalisha umeme ambapo kila mmoja ina uwezo wa kuzalisha megawati 235 nalo limekamilika kwa asilimia 99.

Msigwa amesema sehemu nyingine ambayo imetiliwa mkazo ni  utekelezaji wa Mradi wa kusafirisha umeme kutoka JNHPP hadi Chalinze wa kilo voti 400, yenye urefu wa km 160 ambao sasa umefikia asilimia 99.5 ikilinganishwa na asilimia 44 mwaka 2021/22.

Aidha, ujenzi wa kituo cha kupoza Umeme cha Chalinze ambacho ni sehemu ya mradi huo umefikia asilimia 92 ikilinganishwa na asilimia 35.9 mwaka 2021/22. Ukamilishwaji wa miundombinu hii imewezesha umeme kusafirishwa kutoka kituo cha kuzalisha umeme cha JNHPP hadi Chalinze na kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa.


Msigwa amesema thamani ya ujenzi wa Mradi wa JNHPP ni Shilingi tririon 6.558 ambapo hadi kufikia mwezi Februari 2025, mkandarasi alimelipwa kiasi cha Shilingi Bilioni 6.3 ambacho ni sawa na asilimia 95.9.

Amesema kukamilika kwa mradi huo ni mingine inayoendelea nchini utasababisha nchi kuzalisha umeme mwingi wa mege wati 4000 wakati mahitaji ya ndani ni mege wati 1900 hivyo kuwa na umeme unaoweza kuuzwa nje ya nchi ikiwa ni pamoja na Zambia na Kenya.

Post a Comment

0 Comments