Na: Siwema Malibiche
Wanafunzi
wapya waliochaguliwa kujiunga na masomo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)
kwa mwaka wa masomo 2024/2025 wametakiwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa
huku wakisoma kwa bidii zitakazowawezesha kutimiza malengo yao waliyojiwekea.
Hayo
yamebainishwa na Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda wakati
wa kufunga wiki ya mapokezi ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza iliyofanyika ndani
ya Kampasi ya Solomon Mahlangu mkoani Morogoro ambapo amewataka wanafunzi hao
kuishi katika malengo waliyojiwekea huku akisema Menejimenti ya SUA imeandaa
miondombinu bora ya kujifunzia na itaendelea kuboreshwa.
Aidha
amesema uongozi wa Chuo hautafumbia macho vitendo vyovyote vinavyoashiria ukatili
wa kijinsia chuoni hapo na ameongeza
kuwa sheria kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo
vya ukatili wa aina yoyote huku
akiwahasa wanafunzi wote kuishi katika maadili yanayostahili kwa jamii.
Naye
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Mipango, Utawala na Fedha SUA Prof. Amandus Muhairwa amesema
SUA itaendelea kujenga na kuboresha miundombinu kupitia mradi wa HEET katika kampasi zake zote kwa kuzingatia
mahitaji ya watu wenye ulemavu ili kuboresha mazingira ya kujifunzia.
Aidha
amewataka wanafunzi wote ambao ni wanufaika na mkopo wasisite kufika katika ofisi za mikopo chuoni
na jumuiya ya wanafunzi chuoni hapo
wanapopata changamoto yoyote ya kifedha
ili kupata ufumbuzi wa haraka na
wenye kuepusha madhara ambayo yanaweza kujitokeza kutokana na wanafunzi
kutotoa taarifa.
Kwa upande wake Rasi wa Ndaki ya Sayansi za Jamii na Insia SUA Prof. Samwel Kabote ambaye amemwakilisha Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Maulid Mwatawala amesema wanafunzi waliochagua kujiunga na masomo SUA wamefanya chaguo sahihi kutokana na Chuo hicho kuwa na mazingira mazuri ya kusoma ikwemo maktaba, itakayowawezesha kusoma machapisho mbalimbali, huduma za afya na ulinzi madhubuti na ni vyema kutumia ipasavyo.
Nao wanafunzi wa mwaka wa kwanza Bw. Daudi Adrea na Bi. Laura Koka ambao ni wanafunzi waliojiunga na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo wameupongeza uongozi wa Chuo hicho kwa maandalizi mazuri ya kuwapokea huku wakiwataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii na kuepukana na makundi mabaya yatakayowafanya kutotimiza malengo yao.
0 Comments