Na: Calvin Gwabara – Dodoma.
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
kimedhamiria kuwa mstari wa mbele kwenye kufanya tafiti mbalimbali kwa kutumia
teknolojia ya Bioteknolojia ili kusaidia kupata majibu ya kisayansi kuhusu
faida na hasara za teknolojia hiyo nchini kwa kutumia wataalamu wa ndani.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda wakati akichangia kwenye mjadala huyo wa Bioteknolojia kwenye mkutano wa CROSAT jijini Dodoma. |
Kauli hiyo imetolewa na Makamu Mkuu
wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda wakati akizungumza kwenye jopo la watafiti
wabobevu wa teknolojia hiyo kutoka Tanzania, Ubelgiji na Kenya kweye mkutano wa
Chama cha Wataalamu wa Sayansi za Mazao Tanzania (CROSAT) jijini Dodoma wakati
wa mjadala maalumu ulioangalia mchango wa Bioteknolojia kwenye uboreshaji wa
mazao, mtazamo wa kidunia kwenye sayansi za bioteknolojia kwenye uboreshaji wa
mazao.
“Sisi kama Chuo tegemeo la nchi kwenye
masuala ya Tafiti za kilimo na sayansi zinazoendana na kilimo tumeshapeleka
maombi serikalini ili Chuo chetu kiwe moja ya vituo vya umahiri vitatu
vinavyoanzishwa na Serikali kwa ajili ya kufanya tafiti za bioteknolojia ili
tusaidie nchi kubaini ukweli kuhusu teknolojia hiyo kwa undani ili iweze
kusaidia nchi” , amesema Prof. Chibunda.
Amesema kuwa Tanzania na nchi
zingine za Afrika kutopiga hatua kwenye matumizi ya teknolojia hiyo kunatokana
na kutoifahamu na kauli za vitisho vya baadhi ya watu wanaopinga hali
iliyopelekea Tanzania kujiwekea sheria na kanuni ngumu ambazo zinawafunga
mikono watafiti wake kushiriki kikamilifu katika kuitumia na kuleta maendeleo
ya watanzania na Taifa katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili.
“Ni maombi ya wanasayansi kwamba
muda umefika sasa wa nchi zetu za Afrika na Tanzania ikiwemo kuangalia upya tunawezaje
na sisi kushiriki kwenye hii teknolojia kama ambavyo tumeambiwa na wenzetu wa
Ubelgiji kuwa nchi za Marekani, China, India lakini pia tumeona nchi za Ulaya
japo hawalimi sana mazao yatokanayo na teknolojia ya Uhandisi jeni lakini ni
watumiaji wakubwa kwa kuwa wanaagiza kutoka katika nchi zinazolima na wanatumia
kwa manufaa ya nchi zao”, ameeleza Prof. Chibunda.
Aliongeza “ Kwa hiyo mimi wito wangu na Chuo chetu kitakuwa mstari wa
mbele kuona ya kwamba katika kuanza na kufanya utafiti ili tuone hata kama
tunasema kuna madhara basi madhara hayo tuyadhihirishe kwa kazi ambayo
imefanywa na watu wetu wenyewe badala ya kutegemea maneno ya kuambiwa au
kutegemea tafiti ambazo zinafanywa nje ya mazingira yetu”.
Awali akitoa wasilisho lake
Prof.Marc Heidje kutoka Taasisi ya Flemish ya Bioteknolojia (VIB) ya Ubelgiji amesema kufuatia ongezeko kubwa la watu duniani, kupungua
kwa maeneo ya kilimo kutokana na makazi, mabadiliko ya tabianchi na uhitaji
mkubwa wa chakula kulisha watu hao nchi nyingi duniani zinatumia teknolojia
hiyo na kusaidia kuongeza uzalishaji na tija kwenye kilimo.
Prof.Marc Heidje kutoka Taasisi ya Flemish ya Bioteknolojia (VIB) ya Ubelgiji akitoa wasilisho lake kwenye mkutano huo. |
“Teknolojia hii sio risasi ya
shaba kwenye kutatua changamoto zote za kilimo bali ni teknolojia nzuri
inayorahisisha uzalishaji wa mbegu kwa kupata sifa zinazohitajika kwa haraka
ukilinganisha na njia za kawaida na hakuna mtu ambaye alishawahi kutoa ushahidi
na kuthibitika kuwa ameyapata kutokana na kutumia mazao yanayotokana na
teknolojia hiyo”, alisema Prof. Marc.
Aliongeza “Kuna maneno mengi ya
uzushi ya kutisha watu kuwa nchi za Ulaya hazilimi wala kula mazao yatokanayo
na teknolojia ya uhandisi jeni lakini niwathibitishie kuwa ubelgiji tunalima na
tunaingiza mazao hayo kwa wingi kutoka nchi zinazolima na nchi nyingi za ulaya
zinalima na kuagiza kwa wingi sana mazao hayo kwa ajili ya chakula cha binadamu
na mifugo”.
Mkutano wa mwaka huu wa Chama cha
Wataalamu wa Syansi za Mazao Tanzania (CROSAT)
umeanza kwa mkutano wa kisayansi uliobeba kauli mbiu isemayo
“Kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia teknolojia za uzalishaji wa
mazao” na kufuatia na Mkutano mkuu wa Mwaka na
umewakutanisha wadau kutoka ndani na nje ya Tanzania.
MATUKIO KATIKA PICHA WAKATI WA MJADALA HUO
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Uthibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania TOSCI bwana Patrick Ngwediagi akichangia kwenye mjadala huo. |
Rais wa Chama cha Wataalamu wa sayansi za Mazao CROSAT Prof. Kalunde Sibuga akizungumza kwenye mkutano huo. |
0 Comments