Na: Calvin Gwabara – Dodoma.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania kupitia Wizara yake ya Kilimo imetenga kiasi cha shilingi bilioni 4
kwenye bajeti ya mwaka 2024/2025 kwa ajili ya ujenzi wa maabara za kisasa za
Bioteknolojia ya kisasa na kuziendeleza kwa manufaa ya Taifa.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi
wa Utafiti na Ubunifu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Dkt.
Deusdedith Mbanzibwa wakati akizungumza kwenye Mkutano wa Chama cha Wataalamu
wa Sayansi ya mazao Tanzania (CROSAT) wakati wa mjadala uliokutanisha jopo la
wataalamu wa Bioteknolojia kutoka Tanzania, Kenya na Ubelgiji wakiangalia nafasi
ya teknolojia hiyo kwenye uboreshaji wa mazao nchini.
“Wizara ya kilimo imekuwa
ikitenga fedha nyingi kila mwaka kwa lengo la kuimarisha miundombinu ya tafiti
za bioteknolojia na teknolojia nyingine lakini Bioteknolojia imekuwa ikitumika
nchini kwenye kufanya kazi mbalimbali ikiwemo utambuzi wa magonjwa, Wadudu na
uzalishaji wa miche kwa njia ya chupa, hivyo ujenzi wa maabara hizo kubwa pale
kwenye kituo cha utafiti wa Kilimo Mikocheni utasaidia kuimarisha utumiaji wa
teknolojia hiyo nchini”, alieleza Dkt. Deusdedith.
Amesema sambamba na hilo Serikali
kwa kushirikiana na wadau wengine wa kilimo wamewezesha watafiti kwenye kila
kituo cha TARI nchini kwenda kusomea na kupata utaalamu wa teknolojia hiyo na
hivyo kusaidia kuwa na wataalamu wa kutosha na wengi wao wapo kwenye kituo cha
TARI Mikocheni ambapo ndiyo tafiti zinazotumia teknolojia hiyo zinafanyika.
Kwa upande wake Mtafiti Mkongwe
wa Bioteknolojia nchini kutoka Chama cha Wataalamu wa Bioteknolojia Tanzania
(BST) Dkt. Nicholous Nyange amesema kuwa kikwazo kikubwa cha kutosonga mbele
kwa teknolojia hiyo nchini ukilinganisha na nchi zingine na Kanuni iliyowekwa
kwenye sheria ya Mazingira ambayo inatoa nafasi kwenye kufanya tafiti lakini
inawafunga watafiti mikono kufikisha bidhaa za teknolojia hiyo sokoni.
“Tanzania imeweka kanuni, miongozo
na sera za kusimamia matumizi ya teknolojia hii hapa nchini lakini kifungu
kimoja kwenye kanuni ya sheria ya mazingira ndiyo kikwazo cha ubiasharishaji hivyo tunaiomba Serikali kufikiria upya
kanuni hiyo ili iwezeshe wanasayansi kusaidia kwa haraka kutatua changamoto
nyingi zinazowakabili wakulima na kwenye sekta nyingine kutumia teknolojia hiyo
wakati ikijiandaa na ujenzi wa maabara hizo”, alieleza Dkt. Nyange.
Naye mtaalamu kutoka Mamlaka ya Uthibiti wa Mimea na Mazao ambaye amebobea kwenye masuala ya Sera, kanuni na miongozo ya bioteknolojia kutoka nchini Kenya Dkt. Anne Muia amesema kuwa ni muhimu teknolojia za kisasa zitumike kwenye kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili wakulima na kwenye sekta zingine.
“Mimi kama jirani wa Tanzania
lakini mmoja wenu hapa Afrika nasema kuna umuhimu mkubwa sana wa kuhakikisha
wananchi wetu wanakula wanashiba na nchi kujitosheleza kwa chakula utaona
teknolojia tulizokuwa tukizitumia miaka 100 iliyopita kwa sasa zinaanza
kushindwa kufanya kazi vizuri hivyo ni muhimu sana kwenda kwa wakati na
kukimbizana na mabadiliko haya makubwa ya tabianchi ambayo yanakuja na
changamoto nyingi”, alieleza Dkt. Anne.
Aliongeza “ kama vile tunavyoona
ukuaji wa teknolojia kwenye sekta zingine kama mawasiliano, usafiri na afya
vivyo hivyo wanasayansi wetu duniani pia wanahangaika na kupata teknolojia
mbalimbali za kusaidia kuongeza uzalishaji wa mazao hivyo ni muhimu kuwawekea
mazingira mazuri ya wao kufanya kazi kwa kuwawezesha lakini kusaidia teknolojia
nzuri walizonazo zinatoka maabara na kwenda kunufaisha jamii na Taifa”.
Dkt. Anne amesema wao kama
wasimamizi wa teknolojia hizo nchini Kenya kazi yao sio kuzuia teknolojia nzuri
za watafiti wao bali kuweka mazingira mazuri ya kuzikagua, kuzifuatilia
kuhakikisha zipo salama kwa watu na mazingira na kuzipa nafasi ya kufika kwa
wananchi na kuwanuifaisha.
Chama cha Wataalamu wa Sayansi za
Mazao nchini CROSAT wameweka mada hiyo na mjadala huo uliowakutanisha wataalamu
wabobevu kutoka Tanzania, Kenya na Ubelgiji kwa lengo la kupeana uzoefu kama
wataalamu wa mazao na kujadiliana kwa pamoja kuona nafasi ya teknolojia hiyo
kwenye kuboresha mazao na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi hapa nchini.
Muongoza mjadala huo Dr. Ally Mahadhy kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salam akiongoza mahadiliano kwenye jopo hilo. Prof. Raphael Chibunda ambaye ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine akifuatilia mjadala huo. Dkt. Yasinta Nzogela kutoka SUA ambaye ni mwenyekiti wa siku ya majadiliano akizungumza kabla ya kumkaribisha muongoza mjadala huo wa Bioteknolojia. Katibu Mwenezi wa CROSAT Bi. Jenifer Tairo akitoa mchango wake kwenye mkutano huo.
0 Comments