Na:
Farida Mkongwe
Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko
ya Tabianchi na Ustahimilivu katika Nyanda Kavu za Kitropiki (CLARITY)
kinafanya utafiti ili kubaini Teknolojia na nyenzo ambazo zitaondoa kemikali
sumu kwenye maji ya kisima kwa kutumia mimea ambayo inapatikana kwenye jamiii.
Utafiti huo umewekwa bayana na Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili kutoka SUA anayefanya utafiti huo Poliect Onesmo Ngowi wakati akizungumza na SUA Media jijini Dodoma Novemba 18, 2024 katika Warsha ya kuitambulisha Kamati ya Ushauri ya Kimataifa ya CLARITY, warsha ambayo pia imewakutanisha Wasimamizi wa wanafunzi wa Shahada za Uzamili na Uzamivu ambao wapo chini ya mradi huo pamoja na wadau wakuu katika utekelezaji wa mradi wa CLARITY ambao walifanya tathmini ya maendeleo ya mradi huo.
Bw. Ngowi amesema mwisho wa utafiti huo anatarajia kupata teknolojia na nyenzo za gharama nafuu ambazo zitawasaidia watanzania kunyonya vimelea sumu kwenye maji, “ sumu hiyo itakapoondolewa itawawezesha kupata maji safi na salama yatakayowasaidia kufanya afya zao ziwe bora kwani maji yasiyo safi yenye vimelea sumu yanasababisha magonjwa kwa binadamu na wanyama, mimea kufa na mazao kutokuwa vizuri”.
SUA
kupitia mradi huo wa CLARITY pia inafanya utafiti unaohusu athari za mabadiliko
ya tabianchi kwenye upatikanaji wa maji ya chini ya ardhi katika maeneo ya
Nyanda kavu za kitropiki mkoani Dodoma ambao unafanywa na mwanafunzi wa Chuo
hicho wa Shahada ya Uzamivu Evarest Abraham ambaye amesema matokeo ya utafiti
huo yatawezesha katika utungaji wa sera na mikakati mbalimbali ambayo
itawezesha kusimamia rasilimali maji kwa uendelevu na kutengeneza usawa katika
upatikanaji wa maji.
Naye
Mwanafunzi Brenda Mndolwa ambaye pia
anasoma Shahada ya Uzamivu SUA anayefanya utafiti kuhusu upatikanaji wa maji
chini ya ardhi na jinsi maji hayo yanavyoweza kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi
na mabadiliko ya matumizi ya ardhi katika maeneo ya nyanda kavu za kitropiki
mkoani Dodoma ameushukuru mradi wa CLARITY kwa kuwapa ufadhili na kuwataka
waendelee kufanya hivyo kwa wengine kwani bado tafiti nyingi zaidi zinahitajika
katika masuala ya maji ili kusaidia jamii na taifa kwa ujumla.
Kwa
upande wake Prof. Faith Mabiki kutoka Ndaki ya Sayansi Asilia na Tumizi SUA aliyebobea
katika Kemia ambaye ni Msimamizi wa mwanafunzi Poliect Ngowi amesema kuna
umuhimu mkubwa sana wa kuwa na watafiti vijana hasa katika maeneo ya maji
ambayo yanaleta faida katika jamii kwa kuwa vijana wana maisha marefu zaidi
na uwezo wa kuifikia jamii kwa haraka kwa kutumia mbinu mbalimbali za kisayansi na
kitafiti.
Kiongozi Mkuu wa Mradi wa CLARITY Prof. Japhet Kashaigili ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti , Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalam SUA, amesema Mradi unawajengea uwezo wanafunzi ambapo hadi sasa unawafadhili wanafunzi wa Shahada za Uzamivu 2 na Shahada za Uzamili 4, “kimsingi tupo vizuri na tunaendelea vizuri na mradi huu wanafunzi wetu wapo kwenye hatua ya utekelezaji wa tafiti zao kwa kuendelea kukusanya takwimu ambapo tafiti hizo zitachangia kwa kiasi kikubwa mradi huu kufikia malengo yake”.
Mshauri wa Mradi huo kutoka Tanzania Prof. Damas Mashauri amepongeza hatua iliyofikiwa na mradi wa CLARITY na kuahidi kutoa ushauri wake kwa kadri inavyowezekana ili mradi uweze kuwa na mafanikio makubwa “sisi tutashauri huo utaalamu wa kuleta maji kutoka Ziwa Victoria mpaka Dodoma au kuchimba visima kule Mzake kuongeza maji katika mji wa Dodoma ipi itakuwa vizuri, watumie njia gani kwa kuangalia gharama na mazingira wao wataamua kwamba ushauri wauchukue vipi katika utekelezaji”.
Mkuu
wa Kituo Mahiri cha Rasilimali za Maji kutoka Wizara ya Maji Mhandisi Hosea
Sanga amesema kutokana na kuwepo kwa changamoto nyingi zinazoikabili Sekta ya
maji ikiwa ni pamoja na uchafuzi na uvamizi wa vyanzo vya maji “mimi naona kuna
umuhimu mkubwa wa kufanya tafiti hizi na niwaombe wenzetu wa CLARITY kuendelea
kufanya tafiti kwa kushirikiana na jamii kwa karibu zaidi ili matokeo
yatakayopatikana yaende mojakwa moja katika utungaji Sera zitakazoleta tija kwa
jamii”.
Mradi wa CLARITY unafadhiliwa na Kituo cha Utafiti wa Maendeleo ya Kimataifa (IDRC Canada), Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo (FCDO, Uingereza) chini ya mpango wa Kukabiliana na Hali ya Hewa na Ustahimilivu (CLARE).
PICHA ZAIDI BOFYA HAPA CHINI
0 Comments