Na: Siwema Malibiche
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeendesha mafunzo kwa
wanafunzi wake kwa lengo la kuwaunganisha na soko la ajira pamoja na taaluma
zao na Mafunzo yaliolenga kuwapa
wanafunzi taarifa sahihi kuhusu mambo muhimu ya kuzingatia katika upatikanaji
wa ajira.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo anayeshughulikia Mipango, Utawala, na Fedha, Prof. Amandus Muhairwa akizungumza na wanafunzi. |
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika katika Kampasi ya Solomon Mahlangu, Morogoro, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo anayeshughulikia Mipango, Utawala, na Fedha, Prof. Amandus Muhairwa, amesema Tanzania ina fursa nyingi ambazo wanafunzi wanaweza kuzitumia ikiwa watazingatia mafunzo wanayopokea kutoka kwa wadau mbalimbali.
Aidha, Prof. Muhairwa ameeleza kuwa Menejimenti ya Chuo inaendelea kuboresha miundombinu kupitia mradi wa HEET kwenye kampasi zote za SUA ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora. Amesisitiza wanafunzi wasikate tamaa na badala yake waongeze bidii, wawe wabunifu, na kupambana ili kufikia malengo yao ya kujiajiri na kuajiriwa.
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, na Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu, Prof. Japhet Kashaigili, amehimiza wanafunzi wote waliokuwepo kwenye mafunzo hayo kuyafanyia kazi mafunzo wanayopokea kutoka kwa wawezeshaji, akisema kuwa maarifa wanayopata yatasaidia kukidhi vigezo vya kujiajiri na kuajiriwa.
Kwa upande wake, Mratibu wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu SUA, Dkt. Doreen Ndosi, ameeleza kuwa lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwawezesha wanafunzi kuelewa mahitaji ya soko la ajira ili waweze kuajiriwa na kujiajiri katika taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi. Dkt. Ndosi pia amewahimiza wanafunzi kuendelea kutoa mawazo yao ya kibunifu kupitia SUA Innovation Hub, akiahidi msaada kwa mwanafunzi yeyote atakayekuja na wazo la ubunifu.
Mratibu wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu SUA, Dkt. Doreen Ndosi akisisitiza jambo kwa wanafunzi |
Wanafunzi kutoka chuoni hapo walioshiriki mafunzo hayo, akiwemo Bi. Upendo Mwamlima na Bw. Climile Simon, wameipongeza menejimenti ya chuo kwa kuandaa mafunzo hayo. Wameeleza kuwa mafunzo hayo yatakuwa msaada mkubwa katika maandalizi yao ya kutafuta ajira na kujiajiri, na wamependekeza mafunzo kama hayo yaendelee kufanyika kila mwaka.
Mafunzo hayo yameendeshwa kwa ufadhili wa mradi wa HEET, na yameshirikisha wadau mbalimbali inchini wakiwemo Bakhresa Company na Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (TAESA) katika kuwajengea uwezo vijana wanapoanza maandalizi ya utafutaji wa ajira.
0 Comments