Na: Calvin Gwabara – Morogoro.
Utafiti wa awali uliofanywa
kuangalia mbinu za ushirikishi za watafiti na wakulima katika uvumbuzi na uhaulishaji
wa Maarifa na teknolojia za kilimo umebaini kuwa zaidi ya asilimia 70 ya
wakulima hawashirikishwi katika hatua za
awali za ubunifu na tekinolojia na kuchangia kuwa na mapokeo hafifu miongozi mwa
wakulima na kutofanya vizuri kwa maarifa hayo.
Hayo yamebainishwa na Mtafiti Mkuu
Mwenza wa Mradi wa Mbinu Shirikishi za Wanafunzi na Wakulima katika Uvumbuzi na
Uhaulishaji wa Maarifa na Teknolojia za Kilimo
(AGRISPARK) Dkt. Nicholaus Mwalukasa wakati akiwasilisha matokeo hayo ya
awali ya mradi huo uliofanyika kwenye Wilaya ya Morogoro Manispaa, Halmashauri ya
Mvomero na Halmashauri ya Morogoro Mkoani Morogoro.
“Matokeo yetu yamebaini kuwa
wakulima wengi wanashirikishwa wakati tu tafiti au teknolojia imeshakamilika
wao wamekuwa wanashilikishwa zaidi kufanya majaribio pia kuona kama utafiti unafanya kazi kitu ambacho
kinapelekea wakulima wengi kutokuwa na maarifa ya kutosha na uelewa na hivyo
kuwa na mapokeo hafifu ambayo hayaleti tija iliyokusudiwa”, alieleza Dkt.
Mwalukasa.
Aliongeza “Katika utafiti huu
ulihusisha wakulima ambao wamewahi kushiriki katika ubunifu, technolojia au
mradi wowote ambao ulifanywa na watafiti wa kutoka SUA, na hapa tulihusisha
wakulima ambao wapo kwenye miradi au utafiti unaofanyika sasa au ule ambao
ulishafanyika”.
Dkt. Mwalukasa amesema matokeo
haya yanaamaanisha kwamba watafiti wanahitaji kuwashirikisha wakulima zaidi
katika hatua za awali za uundaji wa maarifa na maendeleo ya ubunifu ili
kuhakikisha teknolojia za kilimo zinafaa zaidi, zinapokelewa kwa urahisi na
kuwa endelevu.
Pia amebainisha kuwa ni vyema
watafiti wakashirikiana kwa karibu na Maafisa Ugani na Vikundi vya Wakulima ili
kuimarisha usambazaji na upokeaji wa uvumbuzi wa kilimo, kwani makundi hayo
yana ushawishi mkubwa katika kuwafikia na kuwaelimisha wakulima kwa ufanisi.
Akifungua warsha hiyo na uzinduzi
wa mradi huo wa AGRISPARK, Rasi wa Ndaki ya Sayansi Asilia na Tumizi (CoNAs) Dkt. Geofrey Karugila kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo
hicho Prof. Raphael Chibunda amesema mradi huo ni matokeo ya maono makubwa ya
Chuo katika kuinua watafiti wake hasa wachanga kwa kutenga fedha za ndani ili
wafanye tafiti za kusaidia kutatua changamoto za jamii na taifa.
“Zipo tafiti nyingi ambazo zinafanywa
na watafiti wa SUA kwa kuwa kila mwaka Chuo hutenga kiasi cha shilingi Bilioni
moja kusaidia kufanya tafiti hizo na mradi huu wa AGRISPARK ni sehemu ya
matunda ya fedha hizo za serikali ambazo zinasaidia kuleta ufumbuzi wa
changamoto zinazowakabiliwa watanzania huku zikiwajengea uwezo watafiti wetu
hapa chuoni”, alisema Dkt. Karugila.
Dkt. Karugila
amewataka watafiti kushirikiana na jamii katika kubuni mbinu ambazo zinaweza
kusaidia kuondoa changamoto zao ili jamii iweze kunufaika na kazi kubwa
zinazofanywa nao badala ya kutumia fedha na rasilimali nyingine na kuzalisha
bunifu ambazo hazitatumiwa na jamii.
Kwa upande wake Mtafiti Mkuu wa Mradi
huo wa AGRISPARK Dkt. Philbert Nyinondi kutoka SUA amesema mradi huu umekuwa wa
kipekee kwa kuwa si tu unafadhiliwa na fedha za ndani bali unajibu moja kwa
moja changamoto zinazoikabili jamii.
“Mara nyingi tunapokuwa tunafanya
tafiti ambazo tumefadhiliwa na wafadhili toka nje ya nchi unapewa fedha
kulingana na ajenda ya mtoa fedha au kitu anachokipenda lakini tafiti
zilizofadhiliwa na fedha zetu wenyewe moja kwa moja huwa inakwenda kugusa
maisha ya watu kwa maana tunafanyia utafiti kitu au jambo ambalo moja kwa moja
tunataka kama taifa kwa maendeleo yetu” , alifafanua Dkt. Nyinondi.
Mtafiti huyo Mkuu wa mradi amesema jambo
lingine kubwa ambalo mradi unafanya ni kuwashirikisha zaidi wanafunzi kwenye
utafiti huo ili kuwafanya wanapomaliza wawe wanajua changamoto zinazowakabili
wakulima kuanzia wanapoandaa shamba hadi kuvuna na kufikiria mbinu za kuzitatua
badala ya kwenda na taaluma na mbinu
ambazo haziwezi kusaidia jamii kwenye mazingira fulani.
“Kwa hiyo tunakwenda sambamba
wote kwa pamoja, wakulima, wanafunzi na watafiti kuanzia hizi hatua za awali
kabisa hadi mwisho hatua kwa hatua ili maarifa tutakayozalisha na ubunifu
tutakaoupata yawe ni matokeo yetu wote maana sina haja tena ya kwenda
kumfundisha mkulima maana alikuwa ni sehemu ya huu mchakato hivyo kwa njia hii
tutakuwa na matokeo endelevu kwa wakati wote” alieleza Dkt. Nyinondi.
Amesema mradi huo unalenga
kuangalia namna ambavyo jamii ya wananchi wanaozunguka Chuo Kikuu cha Sokoine
cha Kilimo inavyoweza kunufaika na uwepo wa Chuo hicho lakini matokeo yake
ndiyo yatapelekea mradi kutaka usambazwe nje ya Mkoa wa Morogoro au la.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utafiti
kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia COSTECH Bi. Hildegalda Mushi
amepongeza jitihada kubwa zinazofanywa na watafiti wa Chuo Kikuu cha Sokoine
cha Kilimo katika kutatua changamoto zinawazowakabili wakulima na taifa kwenye
sekta ya kilimo.
Amesema COSTECH kama Taasisi
inayosimamia tafiti na kutoa ushauri kwa Serikali kwenye masuala mbalimbali ya
Kisayansi, teknolojia na ubunifu nchini itaendelea kushirikiana na watafiti
wote nchini na kuunga mkono juhudu zao mbalimbali kwa kuwawezesha kupata fedha
za kufanya tafiti hizo ili zisaidie kuwakomboa watanzania.
![]() |
![]() |
![]() |
![]() |
![]() |
Wakulima na watalamu wa kilimo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero na Halmashari ya Manispaa ya Morogoro wakifuatilia mawasilisho. |
![]() |
Wakulima na watalamu wa kilimo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero na Halmashari ya Manispaa ya Morogoro wakifuatilia mawasilisho. |
0 Comments