Na: Siwema
Malibiche
Wasindikaji
wa chakula nchini wametakiwa kutumia tafiti, teknolojia na maabara zilizopo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ili kukuza ubora wa bidhaa wanazozalisha na kuleta matokeo mazuri kwa mlaji na kupanua
soko lao kibiashara.
Hayo yamebainishwa na Mratibu wa Teknolojia na
Ushauri wa Kitaalam SUA Dkt. Doreen
Ndosi wakati wa warsha ya siku mbili inayofanyika katika Kampasi ya Edward
Moringe Sokoine Mkoani Morogoro inayohusisha wataalamu kutoka SUA, wajasiriamali na wabunifu kutoka kongano mbalimbali mkoani humo.
Dkt. Ndosi amesema
lengo kuu la warsha hiyo ni kupitia kwa kifupi andiko linaloonesha namna gani
watafanya kazi katika Kituo
cha Kiteknolojia cha kusindika chakula.
Aidha Dkt. Ndosi amebainisha
kuwa SUA imeanzisha Kituo cha Kiteknolojia cha kusindika chakula
(Agrifood Technology Station) ambacho kitatumika kama kiwanda cha kuzalisha
mazao ya chakula kwa kusindika chakula kutoka kwa wasindikaji mbalimbali ambapo
kitahusika na usindikaji wa chakula kwa
mazao ya mimea na nafaka kwa kutengeneza unga na bidhaa nyingine.
Amesema
SUA inatarajia kufanya kazi na watu wengi kwa namna tofauti kwa kushirikiana na
kwa kutumia kituo hicho cha kiteknolojia ambapo wajasiriamali wote
wanakaribishwa kutumia wataalamu, tafiti na mashine zinazopatikana chuoni hapo ili kuleta faida
kwa mjasiriamali mmoja mmoja na SUA kama
Taasisi.
Kwa
upande wake Afisa Mratibu wa Tafiti kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na
Teknolojia COSTECH) Bi. Minza Charles amesema wao kama tume wamekuwa na
ushirikiano mzuri na SUA katika kuleta andiko lililowakusanya wajasiriamali na
wabunifu pamoja huku akisema kama taasisi
inawakaribisha wajasiriamali kutumia Kituo cha Kiteknolojia cha
Kusindika Chakula kutoka SUA ili kuboresha uzalishaji wa chakula kwa kutumia huduma zake ikiwemo huduma za
kisayansi na kiteknolojia .
Naye
Mkurugenzi Mtendaji kutoka kongano la uzalishaji wa nafaka mkoani Morogoro Bw. Alexander Jekoniah, ameupongeza uongozi
wa Chuo kwa warsha hiyo na kutoa fursa kwa wajasiriamali kutumia maabara
zilizopo chuoni hapo katika uzalishaji wa bidhaa na anaamini kupitia Kituo cha Kiteknolojia cha kusindika chakula
kutoka SUA itasaidia kutumika kwa virutubisho asilia katika kuandaa unga badala
ya kutumia virutubisho kutoka nje ya nchi.
Kwa
upande wake mjasiliamali kutokea Morogoro
Bi. Esther Muffui ameishukuru
SUA kwa kuanzia warsha hiyo na kukiri kuwa kwa sasa watu wengi
wanatamani kula vyakula vinavyokidhi ubora na amewataka wajasiriamali wote
kutembelea SUA katika Idara ya Sayansi
ya Chakula ili kupata ushauri wa kitaalamu utakao wawezesha kuzalisha bidhaa
zenye ubora stahiki kwa mteja ili kukuza afya.
0 Comments