SUAMEDIA

Kitabu cha Edward Moringe kinatoa maarifa na ujuzi wa uongozi

Na: Farida Mkongwe

Baadhi ya Waandishi walioshiriki kuandika Kitabu cha Hayati Sokoine kiitwacho “Edward Moringe Sokoine: Maisha na Uongozi Wake” kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wameeleza umuhimu wa kitabu hicho na kusema licha ya kuzungumzia historia ya Hayati Sokoine, pia kinatoa nafasi kwa msomaji kuielewa ipasavyo historia ya Tanzania na dhana ya uongozi bora.

Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizindua kitabu cha Edward Moringe Sokoine Maisha na Uongozi Wake , kushoto ni mtoto wa Hayati Sokoine na Balozi wa Tanzania nchini Canada Joseph Sokoine

Waandishi hao akiwemo Dkt. Emmanuel Malisa na Dkt. Onesmo Nyinondi ambao ni Wahadhiri Waandamizi kutoka SUA wamesema Kitabu hicho kimejaa maarifa na tunu ya uongozi wa Hayati Sokoine hivyo kuwasisitiza watanzania wote wakiwemo viongozi  na vijana kujifunza kupitia historia iliyoandikwa katika kitabu cha Hayati Sokoine.

“Umuhimu wa kitabu hiki kwa vijana ni mkubwa kwa sababu pia kinaelezea historia ya nchi yetu kwa mfano vita ya Uganda na Tanzania, vita ya uhujumu uchumi vijana wengi hawajui haya mambo, kitabu kinaeleza vizuri kabila la wamasai lipo namna gani, makuzi ya kiongozi huyu, nini kifanyike ili uwe kiongozi bora, sasa ukiangalia historia ya Hayati Sokoine utakuta kuwa makuzi, elimu, siasa, dini na mambo mengine yamechangia kumfanya kiongozi huyu awe mfano wa kuigwa”, amesema Dkt. Malisa.

“Wito wangu kwa viongozi ni kupata nakala ya kitabu hiki na kukisoma kwa maana kimejaa busara na maarifa makubwa ya kuweza kutuongoza, kitabu kimejitanabaisha kabisa na kueleza ni vipi Hayati Sokoine amekuwa kiongozi bora na ana mchango mkubwa kwa Taifa kwa hiyo kiongozi yeyote atakayekipata kitabu hiki na kukisoma kitamjazia ujuzi wa namna gani anapaswa kufanya ili kuwa kiongozi bora”, amesema Dkt. Nyinondi.

Kwa upande wake Afisa Utumishi Mkuu kutoka SUA Hilda Chigudulu amesema vijana wanapaswa kuhakikisha yale mazuri yote yaliyofanywa na hayati Sokoine yanafanyiwa kazi katika kuleta mabadiliko chanya katika jamii na hilo litawezekana iwapo watajifunza kupitia historia iliyoandikwa kwenye kitabu hiki kwa sababu hawakuwepo enzi za uhai wa Hayati Sokoine.

“Kama ambavyo amesema Mhe. Rais Samia wakati wa hotuba yake ya uzinduzi wa kitabu cha Hayati Sokoine na kuhamasisha vijana kukinunua, mimi kama kijana nimeichukua hiyo kauli na nitahamasisha vijana wenzangu tununue ili kupata elimu na wote tuelimike ili tuweze kuyatenda, kuyaenzi na kuyaishi matendo aliyoyafanya Hayati Sokoine”, amesema Chigudulu.

Post a Comment

0 Comments