SUAMEDIA

Halmashauri ya Mji ya Mbulu imeshukuru SUA kwa kuhamasisha wanafunzi wao kusoma masomo ya Sayansi

Na:George Alexander

Halmashauri ya Mji ya Mbulu Mkoani Manyara imewashukuru wataalam na Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kuwahamasisha wanafunzi wao kupenda na kusoma masomo ya Sayansi ambapo imeonekana masomo hayo kukimbiwa na wanafunzi wengi.

                    

Hayo yameelezwa na Afisa Elimu Taaluma wa Halmashauri hiyo Bi. Elionora Nkata mara baada ya kupokea ugeni wa wataalam wanne kutoka  SUA kwa lengo la kuhamasisha wanafunzi hususani wa kike kupenda na kusoma masomo ya sayansi ambayo yameonekana ni tatizo kwa wanafunzi wengi.

Bi. Nkata ameeleza kuwa asilimia kubwa ya wanafunzi ukata tamaa kwenye michepuo yao wanayosoma hususani ule wa masomo ya kemia, bailojia na jiografia wakiamini kuwa mchepuo huo hauna masomo ya kusoma chuo kikuu zaidi ya ualimu hivyo kupelekea wanafunzi wengi kufanya chini ya kiwango na hata wengine kubadili mchepuo na wengine kuchagua masomo ya sanaa wafikapo chuoni.

“Wanafunzi wengi wamekuwa wakikata tamaa hususani wanaochukua mchepuo wa CBG maana wamekuwa wakiamini hakuna kozi nyingine wakifika chuo watakayosoma kupitia mchepuo huo tofauti na Ualimu, binafsi nawashukuru sana SUA kwa kuja sababu wanafunzi wametiwa moyo” amesema Afisa Elimu huyo.

Ameongeza kuwa katika wilaya yake jumla ya shule 15 kati ya 21 zinafundisha somo la kilimo hivyo imekuwa faida kubwa kwa wilaya na kwa wanafunzi kwa sababu wanafunzi wamepata kuelekezwa kozi mbalimbali zinazotolewa SUA na ufaulu ambao unatakiwa hivyo itachochea wanafunzi wengi kusoma kwa bidii.

Aidha kwa upande wao walimu wameonekana kufurahishwa na kuvutiwa na kile kinachofanywa na SUA kwa kuwatumia wataalam wake ambao ni mabinti wadogo waliopata mafanikio kuja kuzungumza na wanafunzi wao ambao wanakutana na vikwazo vingi vya kuzuia ndoto zao, ikiwemo mimba na wengine kukatisha masomo yao kwa kuona wanapoteza muda.

 “Wanafunzi wa ukanda huu wengi wana uwezo sana wa masomo ya Sayansi na wengi huwa wanafaulu, lakini huwa tunashangaa wafikapo kidato cha tano na sita baadhi uwezo wao hupungua na wengine wafikapo vyuoni huchagua kozi za masomo ya sanaa” amesema mwalimu Shija Chile ambaye ni mwalimu wa somo la baiolojia katika shule ya Chief Salwat.

Kwa upande wao wanafunzi wamewashukuru sana SUA kwa kuwakumbuka na kufika katika shule zao huku wakieleza kutibiwa majeraha yaliyokuwa yakiwasumbua kichwani mwao ya kuweza kusoma masomo ya Sayansi lakini kutokana na kutokuwa na uelewa huamua kusoma masomo mengine tofauti na masomo ya sayansi.

Lucia Faustine ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya sekondari Tlaw iliyopo wilayani humo amesema ameshawishika sana kuona wataalam na wahadhiri wenye umri mdogo ambao wamepata mafanikio yao kupitia masomo na kutokupoteza muda na hata wengine kuwa na taaluma mbili kama Daktari na Mhandisi.

Mwanafunzi huyo ameahidi atajitahidi ili aje afikie malengo yake ya kusoma masomo ya sayansi na kubainisha kuwa kupitia wataalamu hao amejua masomo ya Sayansi yana fursa nyingi za ajira nchini.

SUA kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi yaani HEET inaendesha programu maalum ijulikanayo kama STEMI yaani Science, Technology, Engineering, Mathematics and Innovation kwa awamu ya Pili katika Mkoa wa Manyara na Singida huku lengo likiwa ni kuwafanya wanafunzi wengi kusoma masomo ya Sayansi, Teknolojia na Uvumbuzi.





Post a Comment

0 Comments