SUAMEDIA

Afrika ya Kusini kushirikiana na SUA ili kuleta maendeleo ya kilimo

 Na Gerald Lwomile

Serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kusini kupitia Wizara yake ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu imesema mashirikiano katika Sayansi, Teknolojia na Ubunifu baina ya Tanzania na Afrika ya Kusini yataleta maendeleo kati ya pande hizo mbili.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda kushoto akimpa zawadi Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kutoka Afrika ya Kusini Dkt. Bonginkosi “Blade” Nzimande (Picha zote na Ayoub Mwigune)

Hayo yamesemwa Oktoba 30, 2024 na Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kutoka Afrika ya Kusini Dkt. Bonginkosi “Blade” Nzimande wakati akizungumza na viongozi na menejimenti ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo alipofanya ziara yake ya siku moja chuoni hapo.

Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kutoka Afrika ya Kusini Dkt. Bonginkosi “Blade” Nzimande na ujumbe wake wakiwa katika ofisi ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda

Dkt. Nzimande amesema ni muhimu kuwepo kwa ushirikiano kati ya nchi yake na SUA katika maeneo mbalimbali kama Utafiti, Teknolojia na Program za kubalishana uzoefu kwa wanafunzi na wataalamu ili kuhakikisha kunakuwa na maendeleo katika sekta ya kilimo na kuleta maendeleo kwa watu wake.

Waziri huyo wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu amesema endapo nchi hizi mbili zitafanya tafiti mbalimbali kwa pamoja zinaweza kuja na matokeo ambayo si tu yatazisadia nchi hizo mbili bali Afrika kwa ujumla.

Amesema Serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kusini itaangalia uwezekano wa kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi kutoka Afrika ya Kusini kuja kusoma katika vyuo vilivyopo Tanzania ikiwa ni pamoja na SUA.

Awali akijibu hoja zilizoibuliwa na Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu wa Afrika ya Kusini na Bi. Linaliwe Gama na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara hiyo Bi. Karabo Mlambo waliotaka kujua kwanini hawaoni wanafunzi kutoka Afrika ya Kusini wanaosoma SUA, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda amesema SUA imekuwa ikipokea wanafunzi kutoka nchi za Botswana, Lesoto, Mozambique na maeneo mengi yaliyoko Kusini mwa Jangwa la Sahara.


Amesema ni matumaini yao kuwa katika siku za usoni watapata wanafunzi kutoka Afrika ya Kusini na hasa kama wataondoa mtazamo hasi wa  elimu inayotolewa katika vyuo vya Tanzania ikiwa ni pamoja na SUA kwani chuo hicho kinafanya vizuri kwa kufundisha na kutoa wataalamu mbalimbali katika maeneo mengine ya Afrika.

Amesema endapo kutakuwa na ufadhili unaotolewa kwa wanafunzi kutoka Afrika ya Kusini watakuja na kupata elimu na ujuzi bora na huenda hata wakatamani kubaki nchini kutokana na kuwepo kwa mazingira mazuri ikiwa ni pamoja na amani na utulivu uliopo.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi na Teknolojia na Ubunifu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia nchini Prof. Ladislaus Mnyone amesema endapo ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Afrika ya Kusini katika Sayansi, Teknolojia na Ubunifu utaboreshwa basi utaleta maendeleo kwa pande zote mbili

Amesema wao kama Wizara wamefurahishwa na ziara hiyo ya Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kusini na kuwa itaimarisha ushirikiano baina ya pande hizo mbili.




Post a Comment

0 Comments