Na: George Joseph
Umoja wa Nchi za Afrika Mashariki umeombwa kuwa wafadhili wakuu wa kudumu katika tafiti mbalimbali zinazofanywa na wataalamu kutoka katika vyuo vikuu vilivyopo katika umoja huo.
Hayo yamesemwa na Prof. Samuel Kabote baada ya majadiliano na tume ya kupitia mabadiliko ya sera ya
Elimu kutoka wizara ya elimu Nchini Uganda waliofika chuoni hapo wakiongozwa na
mwenyekiti wake Mheshimiwa Amanya Mushega kwa lengo la kujifunza mambo
mbalimbali yahusuyo mitaala na tafiti
Prof. Kabote ambaye amemuwakilisha Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, amebainisha
kuwa moja ya vitu ambavyo wamejadili na tume hiyo ilitaka kujua ni wapi chuo
hicho kinatoa pesa kwa ajili ya kufanya tafiti zake. Hivyo wameuomba Umoja huo
wa Afrika Mashariki kuwa uwe chanzo cha kuwawezesha watafiti kutoka katika vyuo
mbalimbali kufanya tafiti zao, kuliko kuwategemea watafiti kutoka sehemu
nyingine ambao mara nyingi hutaka tafiti zao zifanywe kulingana na malengo yao
tofauti.
Naye
Mheshimiwa Amanya Mushega ambaye ni mwenyekiti wa tume hiyo kutoka katika
wizara ya Elimu Uganda amesema lengo la
wao kuja Tanzania na pia Chuo Kikuu cha Sokoine ni kwa sababu ya kujifunza
mambo yahusuyo Mitaala pamoja na utafiti lakini pia ujirani uliopo kati ya
Tanzania na Uganda kwa lengo la kutengeneza na kuboresha sera ya Elimu nchini
Uganda na kuwa sera inayoendana na umoja uliopo wa nchi za Afrika mashariki.
Mheshimiwa
Amanya amesema wamefurahi sana kufika chuoni hapo na kuona namna Chuo hicho
kinavyofanya miradi yake mbalimbali na kuwaingizia mapato. Amesema moja ya
sehemu ambayo wamefurahishwa nayo ni hospitali kuu ya rufaa ya Wanyama iliyopo
katika chuo hicho inavyofanya kazi ya kutibu Wanyama mbalimbali.
Pia
amesema amefurahishwa na namna chuo hicho kinavyofanya mapitio katika mitaala
yake ya kufundishia na kuwa itasaidia kuendana na mabadiliko ya Sayansi na Teknoljia
na pia mabadiliko ya mahitaji mbalimbali katika jamii ikiwemo kilimo na
ufugaji.
Akizungumza
mara baada ya kuwapokea ofisini kwake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Fedha, Mipango
na Utawala Profesa Amedeus Muhairwa kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo Profesa
Raphaeli Chibunda amewakaribisha chuoni hapo na kuwataka wawe huru kuuliza
mambo mbalimbali kwa wataalamu waliopo chuoni hapo ili waweze kufanikisha
malengo ya mchakato wa mabadiliko ya sera ya elimu nchini kwao.
Tume hiyo yenye wataalam pamoja watafiti mbalimbali kutoka Wizara ya Elimu Nchini Uganda imeongozwa na Mwenyekiti wake Mheshimiwa Amanya Mushega na wenyeji wao kutoka kutoka wizara ya Elimu Sayansi Teknolijia ya Tanzania wamefika Chuoni SUA na kupata nafasi ya kutembelea katika sehemu mbalimbali za kufundishia chuoni hapo ikiwemo hospitali ya taifa ya rufaa ya Wanyama.
0 Comments