Na: Calvin Gwabara – Tabora.
Taasisi ya Utafiti wa Tumbaku
nchini (TORITA) imechangai kuongeza mara dufu uzalishaji wa zao hilo tangu
kuanzishwa kwake mwaka 2000 na kuongeza ubora wa zao hilo, hivyo kuinua kipato
cha wakulima na pato la Taifa hasa fedha za kigeni.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi
wa Taasisi ya Utafiti wa Tumbaku Tanzania (TORITA) Dkt. Jacob Bulenga Lisuma
wakati akizungumza na SUAMEDIA kuhusu mchango wa taasisi hiyo tangu kuanzishwa
kwake na mikakati waliyonayo katika kufikia malengo makubwa ya Kitaifa kuhusu
zao hilo.
“Taasisi yetu ya TORITA imetoa
mchango mkubwa sana kwenye uzalishaji wa Tumbaku nchini ambapo mwaka jana 2022
tulizalisha mbegu bora nyingi na kuziuzia kampuni ambazo ziliweza kuzalisha
tani milioni 125 tofauti na mwaka juzi ambapo uzaishaji ulikuwa tani milioni 65
tu” alieleza Dkt. Jacob.
Amesema ukifuatilia zao la
Tumbaku kabla ya kuanzishwa kwa TORITA, kuanzia mwaka 2000 kurudi nyuma
uzalishaji ulikuwa chini ya tani milioni 20. Baada ya mwaka 2000 uzalishaji
ulianza kupanda na kuwa tani milioni 25, 35, 60, 85, 90 na hadi kufikia tani
Milioni 125 za mwaka jana.
Amesema kuongezeka kwa uzalishaji
huo kunatokana na mbegu bora walizozifanyia utafiti na kuzizalisha kwa wingi
kupitia taasisi yao hasa baada ya kutoridhishwa
na uzalishaji haba katika eneo husika ambalo lilikuwa tatizo kwa
wakulima wengi. Wengi wao uzalishaji wao ulikuwa ni mdogo kutokana na kulima
kwa kutumia mbegu za asili na bila kufuata kanuni bora za kilimo cha Tumbaku.
Juhudi za TORITA katika kuongeza
uzalishaji zinachagizwa na ilani ya Chama Tawala na maelekezo ya Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mathalani, “Ilani ya Chama cha Mapinduzi
inatutaka ifikapo mwaka 2025/2026 tuweze kufikia lengo la kuzalisha Tani
milioni 200 za Tumbaku na ukiangalia msimu uliopita tulikuwa na tani milioni
125 hivyo bado tuna upungufu kidogo kufikia kiasi hicho ambacho tunaamini
tutakifikia” Alifafanua Dkt. Jacob.
Mkurugenzi huyo wa TORITA
ameishurkuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa kuongeza fedha za utafiti kwenye taasisi hiyo ambapo milioni 500
zilitumika mwaka wa kwanza kwenye kuzalisha mbegu bora za Tumbaku na kununua
vifaa vya mabaara ambavyo vinasaidia kuhakikisha vinasaba vya mbegu bora
vinachukuliwa ili kuzalisha mbegu bora na zenye sifa zinazohitajika pamoja na
ununuzi wa trekta na magari mawili.
Aidha Dkt, Jacob amesema ni
dhamira yao kuhakikisha wanasaidia kuongeza tija ya uzalishaji wa Tumbaku
nchini kwakuwa ni moja kati ya mazao ya biashara ambayo yameweza kutoa mchango
mkubwa kwenye kuongeza pato la Wananchi na Taifa kwakuwa amaanini takwimu za
mwaka huu zikitoka linaweza kuwa zao linaloongoza katika kuingiza fedha za kigeni.
Ametumia nafsi hiyo pia
kuishukuru wizara ya Kilimo kupitia kwa Waziri wake Mhe. Hussein Bashe na mwenyekiti
wa Bodi ya TORITA Prof. Gration Rwegasira (Wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha
Kilimo) kwa ushirikiano mkubwa wanautoa katika kuhakikisha Taasisi hiyo
inafikia malengo yake.
Mkurugenzi huyo amesema pia
katika kufikia malengo ya Progamu ya BBT pia Taasisi yake imekuwa ikisaidia
vijana wengi kuweza kuingia kwenye shughuli za kilimo ili ifikapo mwaka 2030
kilimo kiweze kuchangia asilimi 10 kwenye pato la taifa kupiti ajenda ya 2030.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
bodi ya Wakurugenzi wa TORITA nchini, Prof. Gration Rwegasira wa Chuo Kikuu Cha
Sokoine Cha Kilimo amesema, TORITA ni Taasisi ya Utafiti ambayo imejipanga vvema
kutimiza malengo yake kama yalivyoainishwa katika mpango mkakati wa mwaka
2021-2026.
Amesema kwakuwa TORITA iliasisiwa
katika Misingi ya ushirikiano wa serikali na sekta binafsi yaani (Public
Private partnership-PPP), imekuwa Taasisi ya mfano wa kuigwa ambayo inazingatia
mahitaji ya Wakulima wakubwa na wadogo, Vyama vya ushirika wa Tumbaku,
Makampuni ya ununuzi wa tumbaku na mifumo ya uendeshaji ya Serikali ili kuleta
ufanisi na kuongeza pato la taifa.
“Tunajivunia ushirikiano mkubwa uliopo kati ya
wadau za zao la tumbaku na Taasisi ya Utafiti wa Tumbaku Tanzania pamoja na
Bodi ya Tumbaku ambao kwa pamoja wamewezesha kuimarisha uzalishaji wa zao hili
na kuongeza tija kwa wakulima na kuinua pato la Taifa.” alisema Prof.
Rwegasira.
Aidha Mwenyekiti huyo wa bodi ya itanabaisha
kwamba, TORITA ni Taasisi pekee nchini ambayo
uongozi wake wa Bodi ya Wakurugenzi, pamoja na wadau wengine,
unazingatia uwepo wa Chuo Kikuu cha Sokoine Cha kilimo (SUA) kama msingi mkuu
wa kuhuisha utaalamu na teknolojia za kisasa kwa faida ya wakulima na umma wa
watanzania.
“Namshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania na Serikali yake yote hasa kupitia Wizara ya Kilimo,
kwa jinsi wanavyothamini mchango wa TORITA na kuisaidia Taasisi kwa rasilimali
watu, fedha na vitendea kazi, lakini zaidi sana kwa sera nzuri na miongozo
inayotuwezesha sisi Bodi ya Wakurugenzi wa TORITA kuisimamia vema Taasisi hii
ili iweze kuwatumikia wakulima wa Tumbaku na wadau wake nchini Tanzania”
alieleza Prof. Rwegasira.
TORITA imekuwa ikifanya tafiti mbalimbali zenye lengo la kuwasaidia wakulima kulima Tumbaku kitaalamu na kuongeza kiasi cha mazao yanayozalishwa katika kila eneo, tafiti za mbegu bora, rutuba ya udongo, visumbufu vya mimea, mbolea na teknolojia za ukaushaji tumbaku zinazozingatia misingi ya kuhifadhi mazingira.
Mwanamke
akivuna Tumbaku (picha na ILOMarcel
Crozet) |
Muonekano
wa Majengo ya Taasisi ya Utafiti wa Tumbaku Tanzania TORITA. |
Muonekano
wa Tumbaku inayozalishwa kwaajili ya kupata mbegu (Picha na MSUMBA NEWS) |
0 Comments