Na Gerald Lwomile
Jitihada za Serikali katika
kuboresha uzalishaji wa mazao ya kilimo na mazingira ya uwekezaji katika sekta
hiyo, kumepelekea Tanzania kuvutia wawekezaji wengi zaidi katika sekta ya
kilimo katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Akizungumza mkoani Iringa katika
siku ya kuwasilisha matokeo ya utafiti wa ‘Wawekezaji wa Kilimo ni wadau wa
Maendeleo?’ (AIDA), Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa Bw. Elias Luvanda
amesema utafiti huo una manufaa makubwa kwa nchi ya Tanzania.
Amesema utafiti huo uliofanyika
pamoja na kuwa na matokeo chanya katika baadhi ya maeneo, utaisadia Serikali
kuboresha na kuhuisha Sera, Sheria na Miongozo yake iwe rafiki kwa wawekezaji
na wadau wa kilimo ili kuakisi uhalisia kwenye mazingira ya nchi.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa Bw. Elias Luvanga akifungua warsha ya uwasilishaji wa matokeo ya utafiti |
Akizungumza mara baada ya
wasilisho la matokeo ya utafiti huu, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili,
Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalam Prof. Esron
Karimuribo amesema matokeo ya utafiti yameonyesha wazi mchango mkubwa na sera
nzuri za uwekezaji za Tanzania.
Amesema kutokana na hali hiyo
imepelekea wawekezaji kuwa na sehemu yao katika kutoa ajira japo si kwa kiwango
kinachotarajiwa, pia rasilimali maji inapatikana katika maeneo wanayofanyia
shughuli zao.
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalam Prof. Esron Karimuribo akizungumza katika warsha hiyo |
Awali akiwasilisha matokeo ya
utafiti huo, Mtafiti Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)
Dkt. Evelyne Lazaro amesema pamoja na kuwa na lengo mahsusi katika utafiti huo
lakini pia waliangalia uwekezaji na athari zake kwa maendeleo.
Amesema maeneo waliyoangalia
katika eneo hilo ni athari katika upatikanaji wa ardhi, ajira na maendeleo kwa
ujumla, pamoja na kuwa ajira imekuwa moja ya vigezo ili kuwepo kwa uwekezaji
lakini matokeo yanaonyesha ajira ni chache ukilinganisha na matarajio.
“Kwa Tanzania haya mashamba
makubwa hajaathiri sana mambo ya usalama wa ardhi na hii ni kwa sababu Tanzania
tuna taratibu na sheria nzuri tu za mambo ya umiliki wa ardhi kwa wakekezaji na
wananchi” amesema Dkt. Evelyne Lazaro.
Akizungumzia usalama wa chakula
Dkt. Evelyne Lazaro amesema wawekezaji wamechangia kwa kiasi fulani kwani watu
waopata kipato wana uwezo wa kununua chakula hivyo kuleta hali nzuri kwa kaya
ambazo zinazunguka mashamba ya wawekezaji.
Dkt. Lazaro akitoa wasilisho la matokeo ya utafiti |
Naye Prof. Khalmadin Mutabazi
ambaye pia ni Mtafiti Mwandamzi kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)
amesema pamoja na kuwepo kwa nia njema ya uwekezaji lakini kulikuwa mazingira
ya mkulima kunufaiaka na wakati mwingine kutonufaika na uwekezaji.
“Pamoja na kuja kwa fursa mpya
kwa wakulima lakini nao wana mipango yao hivyo fursa inapokuja wanakuwa na
wakati wa kipima na kuona nini kinaweza kuwasaidia zaidi mfano
wakulima wa Iringa na Njombe waliwekeza zaidi katika kilimo cha mbao
lakini sasa wanawekeza zaidi katika kilimo cha parachichi” amesema Prof. Khalmadin
Mutabazi.
Prof. Khalmadin Mutabazi akizungumza katika warsha hiyo |
Naye Dkt. Helle Ravnborg
kutoka Taasisi ya Mafunzo ya
Kimataifa ya Dernmark (DIIS) amesema katika utafiti huo wameona kuna zaidi ya
wawekezaji 100 katika sekta ya kilimo kutoka nchini Dermark ambapo
wamegawanyika katika makundi matatu ambayo ni wawekezaji binafsi, taasisi na
makampuni ambapo wawekezaji binafsi ndiyo wanaonekana wana manufaa zaidi kwa
jamii inayowazunguka tofauti na wale makampuni na taasisi.
Naye mkulima Nicodemus Malley, kutoka
kutoka Kijiji cha Oldeani wilaya ya Karatu mkoani Manyara ameiomba Serikali
kuhakikisha inawasaidia wakulima katika umiliki wa ardhi ili kuondoa migogoro
inayoweza kujitokeza baina yao na wawekezaji.
Amesema limekuwa jambo gumu kwa
wakulima na wananchi wengine kumiliki ardhi lakini serikali inaweza kuwa na
dhamira ya dhati ili kuweka usawa baina yao na wawekezaji ili kuhakikisha
wanainua vipato vyao ikiwa ni pamoja na kusomesha watoto kupitia shughuli za
kilimo.
Akiwasilisha matokeo ya utafiti
huo Mwafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) Festo Maro amesema katika utafiti huo
imeonekana asilimia kumi (10%) ya wakulima wa maeneo Iringa na asilimia kumi na
nane (18%) ya wakulima wa Njombe wamehamasika kutoka kwa wawekezaji
kulima mazao ya soya na parachichi ambayo awali hawakuwa wakiyalima.
Mwafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) Festo Maro akiwasilisha matokeo ya utafiti |
Aidha matokeo hayo yameonyesha
asilimia ishirini na sita (26%) ya wakulima wa Njombe walikuawanabadilishana
taarifa na wawekezaji kuhusu mbegu mpya za mazao na teknolojia mpya za pembejeo
na namna ya kupanda mazao huku Karatu ikiwa ni asilimia moja nukta mbili (1.2%)
na Iringa asilimia kumi na sita (16%).
Katika matokeo mengine utafiti
umeonyesha asilimia sabini na nne (74%) ya wakulima wadogo mkoani Iringa
walipata pembejeo na kemikali kutoka kwa mwekezaji huku Njombe ikiwa ni
asilimia ishirini na sita (26%), matokeo hayo pia yameonyesha kuwa asilimia sitini
na mbili (62%) ya wakulima kutoka Njombe waliingia makubaliano na wawekezaji kulima
mazao kwa kuzingatia kiwango cha ubora katika uzalishaji wa mazao.
Utafiti huu
unaoitwa ‘Wawekezaji wa Kilimo ni wadau wa Maendeleo?’
(AIDA) umetekelezwa na SUA, Chuo Kikuu cha Makerere, Denmark na Taasisi ya
mafunzo ya Kimataifa cha Dermark ukishirikishwa wadau mbalimbali katika maeneo
ya Karatu, Iringa na Njombe na kufadhiliwa na Shirika na Maendeleo la Dernmark
(DANIDA).
Chini ni picha zikionyesha matukio mbalimbali katika warsha hiyo 👇
0 Comments