SUAMEDIA

Fanyeni kazi kwa maslahi ya Taasisi - Prof. Mahonge

 Na Gerald Lwomile

Watumishi wa ngazi zote katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wametakiwa kufanyakazi kwa maslahi ya Taasisi kwani maendeleo ya nchi na mahitaji yao kiuchumi yanategemea uwepo wa Taasisi hiyo.

Prof. Christopher Mahonge akitoa mada katika semina (Picha zote na Gerald Lwomile)

Akizungumza na watumishi wa Kampasi ya Mazumbai iliyopo mkoani Tanga Mwenyekiti wa Kamati ya Kuthibiti Uadilifu (KKU – SUA) Prof. Christopher Mahonge amesema ili nchi iwe na maendeleo inahitaji kuwa na watumishi wanaojituma katika kazi kwa kuzingatia uadilifu na kuepuka rushwa.

Amesema ni vyema watumishi wakajua na kufahamu utawala bora ambao umebeba mambo mengi ikiwa ni pamoja na uadilifu, uwajibikaji, uwazi, utawala wa sheria, haki bila upendeleo, ushirikishwaji na kuepuka rushwa.

Prof. Christopher Mahonge aliyekaa (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watumushi wa Kampasi Mazumbai aliyekaa (kushoto) ni Meneja wa Kampasi ya Mazumbai Bw. Steven Kingazi na kulia ni Lightness Mabula Mjumbe wa KKU-SUA

“Uwajibikaji hii ni nguzo muhimu sana, sasa kuna vitu tunavipima kwa uwajibikaji yale majukumu ninayopewa je ninayatekelezaje kufikisha malengo niliyopewa, kwa sababu kuna malengo ambayo tumewekewa kila mtu kwa hiyo uwajibikaji ni muhimu sana” amesema Prof. Mahonge

Akizungumzia ushirikishwaji  kazini Prof. Mahonge amesema pamoja na kuwepo viongozi ambao wana utaalamu katika maeneo yao ni muhimu wataalamu wanaohusika katika maeneo yao wakashirikishwa kumshauri kiongozi na si kiongozi kujiamulia tu kwani anaweza kufanya makosa kwa sababu hana utaalamu katika eneo jingine.

 Kampasi ya Mazumbai

“Na ili uwajibikaji uende vizuri hapa tunajua kila mtu katika kitengo chake anatakiwa afanye nini, kuna kuwajibika kwenda juu? mfano pale juu tuna Meneja wetu, kwa hiyo labda mtu anasimamia kitengo fulani wale wafanyakazi wengine wanatoa taarifa kwa mwingine kwa kufuata ngazi mpaka inamfikia Meneja” amesema Prof. Mahonge.

Akizungumzia mafunzo yaliyotolewa na KKU-SUA Meneja wa Kampasi ya Mazumbai Bw. Steven Kingazi amesema semina iliyofanywa na kamati hiyo ni muhimu kwa watumishi na ameiomba menejenti ya SUA kuhakikisha kamati hiyo inaendelea kwenda katika Kampasi zake kutoa mafunzo kwani mafunzo yatawakumbusha watumishi wajibu wao.

Meneja wa Kampasi ya Mazumbani Bw. Steven Kingazi akizungumza katika semina hiyo

Amesema semina hiyo imetoa hamasa na kuwakumbusha watumishi wajibu wa mtumishi wa umma katika kuhakikisha watumishi wanaenenda katika misingi ya utawala bora.

“Hii inatusaidia kuhakikisha sehemu ya kazi kunakuwa na uwazi, kunakuwa na uzingatiaji wa utawala wa sheria na kanuni za utumishi wa umma, sehemu ya kazi inakuwa siyo sehemu ya kuomba au kupokea rushwa lakini pia sehemu ya kazi inakuwa sehemu jumuishi, kila mtu kwa kada yake na elimu yake anatakiwa kusikilizwa na kuhusishwa katika maamuzi” amesema Kingazi.

Naye Afisa Misitu Bi. Agnes Ngao na mfanyakazi katika Kampasi hiyo Bi. Zubeda Shemmela wamesema mafunzo hayo yamewapa mwanga na uelewa wa mambo na wajibu wa mtumishi katika utekelezaji wa majukumu yake.

Habari picha ya matukio mbalimbali 👇









Post a Comment

0 Comments