SUAMEDIA

Prof. Chibunda ahimiza ushirikiano kutekeleza majukumu Kampasi ya Mizengo Pinda - Katavi

 

Na :Asifiwe  Mbembela

 

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Prof. Raphael Chibunda amewataka watumishi wa Kampasi ya Mizengo Pinda kushirikiana kiutendaji wakati wa kutimiza majukumu mbalimbali ya kiutumishi wa umma.

Prof. Chibunda ametoa wito huo kwa watumishi wa Kampasi ya Mizengo Pinda wakati wa ziara maalum aliyoifanya katika Kampasi hiyo akiwa ameambatana na Menejimenti ya Chuo kwa ajili ya kuwaeleza watumishi hao mipango ya Chuo kwa mwaka ujao wa masomo pamoja na kusikiliza na kutatua kero za watumishi wa Kampasi hiyo.

Prof. Chibunda amewataka Watumishi wa Kampasi ya Mizengo Pinda kushirikiana katika kazi na kuendeleza utamaduni wa SUA kuwa mfano wa kuigwa kwa Jamii inayowazunguka.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Mipango, Fedha na Utawala Prof. Amandus Muhairwa amewahimiza watumishi wa Kampasi hiyo kutosita kufika katika ofisi yoyote pindi wanapokuwa na changamoto yoyote kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi, akiwataka kuacha tabia ya kuziogopa ofisi.

Kwa Upande mwingine Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Maulid Mwatawala amewakumbusha Wanataaluma kuzingatia misingi ya ufundishaji kwa kufuata Utamaduni, Utaratibu na Mwongozo wa Chuo ili SUA iendelea kuwa kitovu cha kuzalisha wanataalamu wenye tija kwa taifa.

Prof. Mwatawala ameongeza kuwa Chuo kipo katika zoezi la kuboresha mtaala wa Chuo, ambapo Kampasi ya Mizengo Pinda wamelenga kuongeza baadhi ya program ambazo zitaongeza idadi ya wanafunzi watakaosoma katika Kampasi hiyo suala ambalo litakuwa chachu katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa jamii inayozunguka Chuo na Mikoa  ya Nyanda za Juu Kusini.

Dkt. Winfred Mbungu, Mratibu wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), akielezea maendeleo ya mradi huo kwa Kampasi ya Mizengo Pinda ambayo itanufaika na ujenzi wa majengo matatu ya kisasa, amesema Mradi huo utakamilika katika kipindi kilichokusudiwa.

Dkt. Mbungu amesema mradi huo unadhamini mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu ambapo amewasihi watumishi wa Kampasi ya Mizengo Pinda kutumia fursa hiyo kujiendeleza kielimu, huku akibainisha baadhi ya watumishi waliopata udhamini wa kielimu kupitia Mradi huo.

Menejimenti ya Chuo imefanya ziara hiyo ikiwa ni mwendelezo wa kufanya ziara ya kuwatembelea watumishi wa SUA katika Kampasi, Ndaki na Shule zao, ili kuwaeleza mipango ya Chuo kuelekea mwaka ujao wa masomo pamoja na kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.

Post a Comment

0 Comments