SUAMEDIA

SUA kushirikiana na Wizara ya Kilimo kuongeza tija katika kilimo kupitia Mradi wa BBT

 

Na : Asifiwe  Mbembela

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimepanga kuanza kuendesha mafunzo tarajali na kutoa ujuzi wa kilimo biashara kwa vijana ili kuweza kuunga mkono juhudi za Wizara ya Kilimo  katika kuinua kilimo kupitia Mradi wa Building a Better Tomorrow (BBT), unaotekelezwa hapa nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam Prof. Maulid Mwatawala aliposhiriki kikao kazi cha Wizara ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa mwishoni mwa wiki iliyopita alipokutana na Makamu Wakuu wa Vyuo Vikuu vya Umma nchini.

Katika kikao hicho upande wa Wizara imewakilishwa na Mratibu wa Mradi wa BBT Bi. Vumilia Zikankuba na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara Bi. Tagie Daisy huku upande wa Chuo mbali na Prof. Mwatawala pia alishiriki Kaimu Mkurugenzi wa Shahada za Awali Dkt. Alex Matofali.

Akiongea katika kikao hicho, Prof. Mwatawala ameahidi kuwa SUA itatoa ushirikiano kwa Wizara kupitia nyanja mbalimbali za kilimo ili kuona vijana wengi zaidi wananufaika na mpango huo kabambe wa kilimo hapa nchini.

"SUA tutashirikiana na Wizara ya Kilimo katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuanzisha kituo cha BBT kwenye Kampasi za SUA; pia tutakuwa tunaendesha mafunzo ya kilimo biashara, mafunzo tarajali na tunakusudia kuongeza uwezo wa kuandika maandiko ya kutafuta rasilimali fedha na watu”, amesema Prof. Mwatawala.

Aidha, ameongeza kuwa Chuo kwa kushirikiana na Wizara kitajikita katika kupima aina za udongo na kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu namna bora ya umwagiliaji ili vijana waweze kunufaika na kilimo kwa kulima kisasa.

Post a Comment

0 Comments