Na
Hadija Zahoro
Watafiti
kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na watafiti kutoka Japan
wamesaini Mkataba wa Makubaliano ili kujadili namna ya kutekeleza mradi ambao
unahusiana na kukabiliana na magonjwa makuu mawili ambayo yanatoka kwa wanyama
kwenda kwa binadamu yanayojulikana kama ugonjwa wa kutupa mimba
(Brucellosis) na Kifua kikuu(Zoonotic Tubeculosis) kwa kutumia dhana ya
afya moja
Mradi
huo utakaotekelezwa baina ya watafiti kutoka SUA utashirikiana na watafiti
wengine Tanzania kutoka NIMR, MUHAS pamoja na vyuo vingine kutoka Japan ikiwemo
Chuo Kikuu cha Rakuno Gakuen na Obihiro ambao utafanyika katika wilaya zote za
Mkoa wa Morogoro.
Akizungumza
na SUA Media mara baada ya utiaji saini wa makubaliano hayo yaliyofanyika
Septemba 19, 2023, Dkt. Coletha Mathew, Mtafiti na Mhadhiri Mwandamizi wa Ndaki
ya Tiba ya Mifugo na Afya ya Jamii katika Idara ya Anatomia na Patholojia,
ambaye amemwakilisha Mkurugenzi wa Mradi huo Prof. Esron Karimuribo amesema
kuwa mradi huo ni muhimu kwa chuo na taifa kwa ujumla kwani unaenda
kukabiliana na magonjwa ambayo yapo katika jamii kwa muda mrefu.
‘‘Sisi
kama SUA tutafaidi kwa maana ya kwamba utafiti huo utazalisha machapisho ambayo
yatakitangaza chuo chetu lakini pia baadhi ya kazi za chuo mbali na kufanya
utafiti na kufundisha lakini pia ni kupeleka huduma za ugani kwa jamii kwa hiyo
jamii itapata uelewa wa namna gani kwa pamoja tutakabiliana na magonjwa
hayo kwa kukubaliana kwa pamoja sisi , jamii pamoja na watafiti wa Japan’’
anasema Dkt. Coletha.
‘‘Mbali
na faida hizo, lakini pia kutakuwa na kipengele cha kujengea uwezo watafiti
wetu wa Tanzania pamoja wanataaluma wetu kwa hiyo SUA pia itafaidika kwa namna
hiyo’’ anaongeza Dkt. Coletha.
Kwa
upande wake Mshauri Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan
(JICA),Dkt. Yumi Kirino ameeleza kuwa ndani ya miaka hiyo mitano ya utekelezaji
wa mradi, wamechagua kwenda kuyafanyia kazi magonjwa hayo mawili ambayo
yanaambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu kwa sababu bajeti ya
kuzuia aina hiyo ya magonjwa haijitoshelezi katika nchi nyingi.
Nae
Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Uchumi na Sekta za Uzalishaji Ofisi ya Mkoa wa
Morogoro, Dkt. Rozalia Rwegasira, ameeleza kuwa Mkoa ni wanufaika wa
mradi huo kwani utakwenda kuwasaidia wananchi wa Mkoa wa Morogoro
kutambua magonjwa hayo na namna ya kujikinga.
Ameeleza
kuwa kutokana na uwepo wa mifugo mingi hivyo kuna matumizi ya mazao ya mifugo
ikiwemo nyama pamoja na maziwa, hivyo mradi huo utakwenda kuacha alama katika
mkoani kwani unakwenda kupunguza athari za magonjwa hayo yanayotoka
kwa wanyama kwenda kwa binadamu.
Mradi
huo unaofadhiliwa na JICA na AMED, utaanza mwezi Julai 2024 na
utatekelezwa ndani ya miaka mitano.
0 Comments