SUAMEDIA

Jimbo Katoliki Tanga, SUA waanzisha ushirikiano wa awali katika Sekta ya Kilimo

 

Na: Hadija Zahoro

Jimbo Katoliki la Tanga kupitia Mradi wao wa kuanzisha Shule ya Sekondari limeanzisha ushirikiano wa awali na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) hasa katika Sekta ya Kilimo kwa lengo la kuwawezesha kupata mafunzo yatakayoifanya shule hiyo kuwa mfano wa kuigwa nchini  kwa upande wa mafunzo kwa vitendo.


Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Wanyama, Ukuzaji Viumbe Maji na Nyanja za Malisho kutoka SUA Prof. Anthony Sangeda amesema ushirikiano huo utaendelezwa  ili  dhana hiyo ya kilimo iweze kufikishwa kwa vijana wadogo ambao wanaweza kuendeleza utaalamu wa kilimo katika jamii na  taifa kwa ujumla.

Prof. Sangeda amesema kupitia Mradi huo Viongozi wa Jimbo Katoliki la Tanga wameona ni vema wajifunze kwenye maeneo ya SUA ili waweze kujua mambo muhimu ya kufanya wanapoanzisha sekondari yao kwani vijana wanaweza kujifunza kwa kushirikiana na Chuo hicho.

“Kimsingi kabisa wageni hawa wana Mradi ambao wanauanzisha katika Jimbo Katoliki la Tanga  ambayo ni Sekondari ya vijana na wanapenda iwe ya mfano kwa nchi hii kwa ajili ya kujifunza kwa vitendo kilimo katika nchi ya Tanzania kwa hiyo wameona ni vyema wajifunze kwa eneo hili la Chuo Kikuu cha Sokojne cha Kilimo”, ameeleza Prof. Sangeda.

Kwa upande wake Padri Gerald Theodol Kabarega kutokea Jimbo Katoliki la Tanga amesema kuwa katika Mradi huo wa Shule, wameona ni vyema kuwa na sehemu  mojawapo ya kilimo ambayo itakuwa chini ya uangalizi wa  Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo ili waweze kujifunza mambo mengi yanayohusu kilimo ambapo yatawasaidia kupata hamu  ya kujiendeleza katika masomo ya kilimo hapo baadaye.

Ameeleza kuwa si tu kuja na elimu ya sekondari ya  kawaida pekee bali kuwe na ujuzi zaidi ya elimu ya sekondari hivyo, wamekuja Chuoni hapo  kuongea na uongozi wa Chuo pamoja na kujifunza mambo ya kilimo na ufugaji na wanaamini kwamba wakifanya makubaliano na Chuo kuweza kusimamia katika Sekta hiyo ya Kilimo na kuweza kuwapa wanafunzi mafunzo mbalimbali basi yataweza kuwasaidia wao na jamii inayowazunguka.

Amesema kuwa mara baada ya kukamilika kwa Mradi huo 2025, kutakuwa na wataalam mbalimbali wa SUA watakaokuwa wanatembelea shuleni hapo na kuwaelekeza masuala ya kilimo katika nyakati tofauti  ambapo pia wanafunzi watapata nafasi ya kufanya ziara Chuoni hapo ili kujifunza kivitendo zaidi.




Post a Comment

0 Comments