Na Asifiwe Mbembela
Jamii imetakiwa kuwa na utamaduni wa kutembelea na kuyagusa maeneo mbalimbali ya watu wenye mahitaji maalum ili kuwa na ustawi wa wananchi katika makundi mbalimbali.
Wito huo umetolewa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Mipango, Fedha na Utawala Prof. Amandus Muhairwa wakati akizungumza na waalimu na baadhi ya wanafunzi wenye mahitaji maalum wa Shule ya Msingi Kauzeni iliyopo Manispaa ya Morogoro Leo tarehe 24 Agosti, 2023.
Prof. Muhairwa ameeleza kuwa kwenye jamii kuna baadhi ya makundi yanahitaji misaada ya namna tofauti tofauti ili kuweza kujikwamua katika vikwazo wanavyokabiliana navyo, akisema kuzitembelea jamii hizo ni kutengeneza ustawi wa kila kundi.
”Tunafahamu sisi tuko hapa lakini kuna maeneo mengine wanahitaji misaada kama hii, tukiwa na utamaduni wa kila mmoja wetu kuyatembelea maeneo kama haya tutakuwa na ustawi mzuri na umoja miongoni mwetu”, alisema Prof. Muhairwa.
Ameongeza kuwa kuisaidia jamii yenye mahitaji ni kuendelea kuunga juhudi za serikali za kutengeneza jamii yenye usawa bila kujalisha mapungufu ya kimwili na kiakili.
Mkurugenzi Menejimenti ya Rasilimali Watu na Utawala Bw. Peter Mwakiluma akiongea katika tukio hilo ameeleza kuwa wametoa msaada huo kama sehemu ya kuwa karibu na jamii pia ni takwa na serikali ambapo inazitaka taasisi zote kuwa na wiki ya utumishi kwa kuigusa jamii na kutoa elimu kwa watumishi katika masuala mtambuka ya kiutumishi.
Mwakiluma ameongeza kuwa msaada ambao wameutoa una thamani ya zaidi ya Tsh 5,200,000 ukijumuisha viti mwendo (Wheelchair), magodoro, mchele, maharage, sukari, vifaa vya kufundishia , mafuta ya kupikia n.k.
Mkwinda Said Chuma Mwalimu wa wanafunzi wenye mahitaji maalum shuleni hapo ameishukuru SUA kwa kutoa msaada huo akisema utasaidia katika kupunguza changamoto zinazoikabili shule hiyo ikiwemo katika kurahisisha ufundishaji wa wanafunzi hao.
Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kauzeni, Yunus Idd Hamis, 12, pamoja na kukishukuru Chuo kwa niaba ya wanafunzi wengine pia ameomba wadau wengine kuendelea kuwasaidia kwani nao wanahitaji kusoma kwenye mazingira rafiki kama walivyo wengine.
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo tangia mwaka 2019 kimeendelea kuadhimisha wiki ya utumishi kwa kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kutoa misaada na kufanya usafi.
0 Comments