SUAMEDIA

Serikali yaipongeza SUA kwa kazi nzuri ya kuendeleza kilimo nchini

 

Na: Farida Mkongwe

Serikali imekipongeza Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kufanya kazi nzuri ya kuendeleza kilimo nchini na kuwataka watanzania kutumia fursa zinazozalishwa na Chuo hicho ili kupata maarifa makubwa zaidi ambayo yatawasaidia kupata maendeleo na kujikwamua na umaskini.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani Jafo akisaini kitabu cha wageni baada ya kutembelea banda la SUA katika Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki mjini Morogoro

Pongezi hizo zimetolewa Agosti 7, 2023 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani Jafo wakati alipotembelea banda la SUA katika Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yanayofanyika mjini Morogoro

“Kubwa zaidi ni kwa watanzania waweze kuona fursa hizi zilizopo katika Maonesho haya, natamani sana watanzania wanaokuja waweze kupita mabanda yote lakini wafike SUA hapa ndipo watapata vitu vingi zaidi, watapata maarifa lakini wengine wataona hata watoto wao wanaowazaa wapi pa kuwapeleka wakapate maarifa zaidi”, amesema Mh. Jafo.

“Maonesho haya yaNanenane nyie ndio mmeyabeba, dhana ya kilimo ndio inapatikana hapa, kwa sababu mbinu za kilimo na tafiti zote zipo kwenu  kwa hiyo niwapongeze sana naona SUA sasa imekuwa sana sio SUA ya wakati ule maana wakati ule hata Idara zilikuwa chache sana, Mkuu wa Chuo nikupongeze sana kwa sababu uongozi wako nao umesaidia kuleta maendeleo katika mambo mengi sana.

Waziri Jafo amesema Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Samia Suluhu Hassan imewekeza sana kwenye Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uuvuvi  ambapo hata kwenye bajeti Rais Samia amefanya mabadiliko na kuongeza bajeti kutoka sh.Bilioni 294.2 kwa mwaka 2021/2022 hadi kufikia sh. Bilioni 970.8 kwa mwaka 2023/2024 na kusema kuwa bajeti hiyo ni mapinduzi makubwa yenye kulenga kuleta mabadiliko chanya katika kilimo.

Waziri Jafo amesema katika kipindi hiki ambapo Rais anafanya uwekezaji huo SUA ina nafasi kubwa sana ya kuwasaidia wakulima kwa sababu ina Teknolojia zote za kisasa na Wataalamu wa kutosha wa kuendeleza kilimo cha Tanzania.

Awali wakati Waziri Jafo akitembelea banda hilo la SUA Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda alimweleza waziri huyo shughuli mbalimbali za Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambazo zinafanywa na SUA kupitia Mabanda yaliyopo kwenye Maonesho hayo ya ya 30 ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Kanda ya Mashariki.


Picha mbalimbali za Waziri Suleiman Jafo akitembelea Banda la SUA








Post a Comment

0 Comments