Na Farida Mkongwe
Wazazi na wanafunzi waliomaliza
kidato cha sita ambao wanatarajia kujiunga na Vyuo Vikuu kwa mwaka wa masomo
2023/2024 wametakiwa kufika kwenye Banda la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)
lililopo katika viwanja vya Maonesho ya
Vyuo Vikuu kwenye viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar Es Salaam ili waweze
kusajiliwa na Chuo hicho.
Afisa Udahili wa SUA Bi. Grace Kihombo (kulia) akitoa maelezo kwa mwanafunzi anayefanya usajili katika Chuo hicho |
Wito huo umetolewa na Afisa
Udahili wa Chuo hicho Bi. Grace Kihombo Julai 17, 2023 wakati akizungumza na
SUAMEDIA katika viwanja hivyo ambapo amesema mwanafunzi akifika katika banda
hilo atapewa elimu kuhusu kozi mbalimbali zinazotolewa na SUA na baada ya hapo
kama atakuwa tayari atasajiliwa moja kwa moja.
“SUA tumekuja na vipeperushi
ambavyo mtu akija hapa anasoma na atachagua kozi ambayo anaipenda kwa hiyo
tunawakaribisha wote ambao wapo karibu na viwanja vya mnazi mmoja waje
tunasajili live kabisa na baada ya
hapo mwanafunzi atakuwa anasubiri kuchaguliwa”, amesema Bi. Grace.
“Kwa hiyo tunawahamasisha
wazazi wote wenye watoto wao ambao wamemaliza kidato cha sita lakini na wanafunzi
waliopo tunawahimiza waje hapa kwenye hivi viwanja vya Mnazi Mmoja ili waje wafanye
maombi maana hapa kuna usaidizi wa kutosha”, amesisitiza Afisa Udahili huyo
kutoka SUA.
Aidha amewataka wazazi na
wanafunzi wanaotarajia kujiunga na vyuo mbalimbali kuelewa kuwa pamoja na kozi
za kilimo, SUA pia kuna kozi za Uchumi na Biashara, Sanaa, Misitu, Wanyamapori
na Utalii na nyinginezo ikiwemo kozi za ualimu ambapo Chuo kinatoa walimu
wazuri wa kozi za Sayansi.
Maonesho ya 18 ya Vyuo Vikuu
ambayo yameandaliwa na Tume ya Vyuo vikuu Tanzania kwa mwaka huu 2023 yamebeba
kauli mbiu isemayo “Kukuza Ujuzi Nchini Kupitia Elimu ya Juu, Sayansi na
Teknolojia kwa Uchumi Imara na Shindani”.
0 Comments