Na: Gerald Lwomile, Dodoma
Imeelezwa
kuwa ili kuleta maendeleo chanya katika sekta ya kilimo nchini, juhudi kubwa
inahitajika kuondoa mitazamo hasi kuhusu kilimo kwa kujenga uelewa kwa wakulima
juu ya kuondokana na kilimo cha mazoea na kujikita katika kilimo biashara,
Serikali kuendelea kuimarisha utengaji na utoaji wa rasilimali fedha pamoja na
kuwepo kwa mashirikiano imara kati ya Wizara Mama za Sekta ya Kilimo.
Dkt. Suzana Nyanda, Mtafiti Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) akiwasilisha matokeo ya utafiti |
Akiwasilisha
matokeo ya utafiti wa Mradi wa SATTA, Aprili 13, 2023 Jijini Dodoma juu ya Ushirikiano ya Wizara Mama za Sekta ya Kilimo katika kuleta Mapinduzi ya
Kilimo Tanzania, Mtafiti kiongozi wa Mradi huo Dkt. Suzana Nyanda, Mtafiti
Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) amesema utafiti wao
umeonyesha kuwa kulikuwa na tofauti kubwa katika utekelezaji wa Mpango wa
Maendeleo ya Kilimo Awamu ya kwanza (ASDP I) na Awamu ya Pili (ASDP II). ASDP I
ilifanikiwa katika kujenga miundombinu ili kuwawezesha wakulima kuzalisha kwa
tija.
Miundombinu hiyo ilijikita katika kuwezesha
uzalishaji mazao, mifugo pamoja Samaki bali ASDP II ilijikita katika kuimarisha
biashara vijijini na uongezaji thamani.
Dkt.
Nyanda amesema katika ASDP I, utekelezaji ulikuwa na mfuko maalumu ambao
ulijumuisha fedha za Serikali pamoja na fedha kutoka kwa Wadau wa Maendeleo. Dkt.
Nyanda amesema zaidi ya kilomita 31,813
za barabara za zilikarabatiwa na zingine kujengwa, masoko 365 ya msingi ya
mifugo yalijengwa, minada ya mifugo ya
upili 46 ilijengwa na viwanda vidogo vya ngozi 336 viliboreshwa.
Ametaja
mafanikio mengine ni pamoja na ujenzi wa skimu za umwagiliaji, vituo vya afya
ya mifugo, majosho, mashine za kukamua mafuta ambayo yote yalipatikana wakati
wa utekelezaji wa ASDP I ambapo maafisa ugani katika ngazi za Halmashauri
washiriki moja kwa moja. ASDP I pia iliwawezesha maafisa ugani na wakulima
kujengewa uwezo katika kuwezesha kilimo chenye tija.
Akizungumzia
matokeo ya utafiti huo kwa upande wa utekelezaji wa ASDP II, Matokeo
yameonyesha kuwa utekelezaji awamu hii unaendelea kufanyika kwa kutumia mapato
ya ndani. Amesema katika mwaka 2021/2022 zaidi ya asilimia 70 ya fedha za Sekta
ya Kilimo zilitengwa kwa ajili ya kuimarisha biashara vijijini na uongezaji
thamani, hii ni pamoja na kuimarisha ushiriki wa Sekata Binafsi katika kilimo.
Hii ni juhudi mkubwa inayofanywa na Serikali ili kuimarisha mnyonyoro wa
thamani katika mazao ya kilimo. Aidha
amesema kuwa mashirikiano ya Wizara Mama za Sekta ya Kilimo ASDP II hayakupewa
nafasi ya kutosha na hata bajeti yake bado haikidhi matarajio. Utekelezaji wa ASDP
II umekuwa na changamoto ya mgawanyo na utoaji hafifu wa rasilimali fedha.
Kwa mwaka 2021/2022, ni asilimia 77.4 tu ya
fedha zilizoidhinishwa zilitolewa. Wakichangia juu ya hilo, wadau waliohudhuria
katika warsha walionyesha umuhimu wa Serikali kuendelea kuboresha mgawanyo na
utoaji fedha katika Sekta ya Kilimo.
Washiriki walieleza kuwa Serikali kuu ipeleke Waraka kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kuwataka kutoa zile asilimia za mapato yatokanayo na uzalishaji wa mazao, mifugo na samaki ili kuwezesha uanzishaji na undelezaji wa miradi ya kilimo katika Halmashauri husika. Kwa sasa fedha hizo zinatolewa kiasi kidogo sana au hazitolewi kabisa hivyo kurudisha nyuma maendeleo katika Sekta ya Kilimo.
Matokeo ya utafiti huo yamewasilishwa kwa wadau wote walioshiriki katika utafiti huo ikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, washiriki kutoka Halmashauri za Njombe na Manyoni pamoja na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo ambacho ndicho kimefanya utafiti huo kwa kutumia mapato yake ya ndani chini ya Mradi wa SATTA-SUARIS1.
0 Comments