SUAMEDIA

SUA yaanza utafiti wa nyasi za asili

 

Na: Winfrida Mwakalobo

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imebainisha kuwa ni wajibu wa kila mdau aliyepo kwenye sekta ya ufugaji kuhakikisha upatikanaji wa malisho na maji ya kutosheleza mahitaji ya mifugo kwa kipindi chote cha mwaka unakuwa ni wa uhakika. 


Hayo yamesemwa na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Charles Mhina wakati akifungua mkutano wa 13 wa wadau wa Nyanda za malisho nchini (RST) uliofanyika mkoani Morogoro Aprili 24,2023.

“Katika miaka ya karibuni takwimu zimetuonesha kumekuwa na tatizo la ongezeko la vifo vya mifugo vilivyotokana na ukosefu wa malisho na maji katika baadhi ya maeneo yaliyokumbwa na athari za mabadiliko ya tabia nchi hivyo kama tusipokabiliana na changamoto hii tutaendelea kupoteza tija kwenye ufugaji wetu” Ameongeza Dkt. Mhina.

Dkt. Mhina ametoa rai kwa Mamlaka za Serikali za mitaa kuendelea kubainisha na kutenga maeneo kwenye halmashauri kwa ajili ya malisho ya mifugo huku pia akiwahimiza wafugaji kununua maeneo yanayokidhi idadi ya mifugo yao, kupanda malisho na kuweka miundombinu ya upatikanaji wa maji ya kutosha.

“Kama kila mfugaji akinunua eneo lake na kulimiliki kwa mujibu wa sheria kisha akapanda malisho ya mifugo yake na kuweka miundombinu ya maji ya kunyweshea mifugo hiyo, tutakuwa tumepiga hatua kubwa kwenye ufugaji wenye tija” Amesema Dkt. Mhina.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha nyanda za malisho nchini (RST) Prof. Selemani Ismail amesema kuwa mkutano huo hulenga kupata maazimio mbalimbali ambayo huwasilishwa kwenye mamlaka mbalimbali ikiwemo Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa ajili ya utekelezaji.

“Nichukue fursa hii kuishukuru Wizara kwani imetekeleza baadhi ya maazimio ya mkutano uliopita ikiwa ni pamoja na lile la uanzishwaji wa mashamba darasa, kutenga maeneo ya malisho, ajira kwa wahitimu wanaomaliza shahada ya usimamizi wa nyanda za malisho na elimu kwa wafugaji wetu ili wafuge ufugaji wenye tija” Amesema Prof. Ismail.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu  cha Sokoine cha Kilimo  (SUA) Prof. Raphael Chibunda ameweka wazi zoezi la utafiti wa nyasi za asili linalofanywa na Chuo chake mara baada ya kugundua mchango wa malisho hayo kwa wanyamapori kwa mwaka mzima.

“waliotutawala walikuja na kuzipa sifa mbaya nyasi zetu za asili japo ndo hizo hizo zinazotumiwa na wanyamapori kama Tembo, Twiga, Pundamilia na wengineo na wakati wote hata kiangazi huwezi kuwaona wanyama hao wamekonda lakini bahati mbaya sisi tumewekeza nguvu nyingi sana kwenye nyasi hizo ambazo ndo zinazowatunza wanyama wetu na ndio maana sisi kama Chuo tumeamua kuchukua hatua” Amesisitiza Prof. Chibunda.

Mkutano huo wa siku moja hufanyika kila mwaka kwa lengo la kujadili kwa kina tasnia ya uzalishaji wa malisho ya mifugo ili kuhakikisha wafugaji wanafuga kwa tija.



Post a Comment

0 Comments