Na: Josephine Mallango
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) katika kuazimisha kumbukizi ya 18 ya Hayati Edward Moringe Sokoine imetoa wito kwa vijana kujifunza kuchukia utegemezi na kutumia fulsa zilizopo hasa katika sekta ya kilimo katika kujipatia ajira.
Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Utawala, fedha na Mipango Prof. Amandus Muhairwa amesema lengo kuu la kumuenzi Edward Moringe Sokoine ni kukiwezesha Chuo kujitathimini jinsi wanavyotekeleza majukumu ya msingi kwa vitendo katika kutoa mafunzo, kufanya tafiti ili kupambana na changamoto za sekta ya kilimo sambamba na kutoa ushauri wa kitaalam kwa wadau mbalimbali .
Aidha Prof. Muhairwa amesema kuwa malengo mahususi ni kukitangaza chuo ndani na nje ya nchi , kutoa fulsa kwa wataaluma na watafiti kujadili matokeo ya tafiti mbalimbali, kuenzi mambo ambayo Sokoine alisimamia utekelezaji wake kwa bidii ikiwemo uadilifu, utii wa mamlaka, kufanya kazi kwa bidii na kupiga vita rushwa ya aina zote sanjari na kusambaza na kujifunza teknolojia mbalimbali za kilimo na ubunifu miongoni mwa wakulima , wafugaji na wavuvi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kumbukizi ya Edward Moringe Sokoine SUA, Prof. Samwel Kabote amesema wataalam wanaozalishwa chuoni hapo siyo tu wanaenda kuwa wanasanyansi tu bali wanakuwa wataalam wa vitendo kwa kufika katika maeneo mbalimbali hasa ya vijijini katika kutoa elimu kwa wakulima wadogo na wakubwa na kusambaza tafiti mbalimbali.
Amesema hiyo inatokana na Hayati Sokoine kuwa kiongozi wa pekee aliyefanya kazi kwa vitendo na kuchukia utegemezi jambo ambalo vijana wote wanapaswa kuliiga katika kutokomeza utegemezi na kutumia fulsa zilizopo na ndio mana serikali imekuja na mkakati wa Building a Better Tomorrow (BBT) kupitia Wizara ya Kilimo unaolenga kuandaa fulsa za ajira kwa vijana katika sekta ya kilimo.
Kwa upande wake Dr. Suzana Samson Nyanda kutoka Ndaki ya Sayansi za Jamii na Insia SUA , amemuelezea Hayati Sokoine alikuwa kiongozi mchapakazi na mzalendo anayefuatilia utekelezaji kwa vitendo na kwamba bado kilimo hakijawa na sura nzuri kwa sasa lakini mikakati inayoendelea inaweza kupelekea vijana kufanya kilimo kwa kuwa hivi sasa vijana wengi wanakwepa kutokana na kuhitaji mafanikio ya haraka ambapo katika kilimo kunahitaji uwekezaji wa muda.
Aidha Maonesho ya Wiki ya Kumbukizi ya Sokoine yamebeba kaulimbiu “Mazingira wezeshi kwa vijana kushiriki katika kilimo sera, miongozo na utendaji “. yataanza Mei 23 hadi 26, 2023 katika Kampasi ya Edward Moringe Sokoine zamani ikiitwa Kampasi Kuu ambapo watanzania wote wanakaribishwa kushiriki na kujifunza na kujionea teknolojia mbalimbali na ubunifu, kushiriki midahalo ya kitaifa , kupata huduma za matibabu kwa wanadamu na mifugo pamoja na michezo mbalimbali ambapo itakuwa ni bure.
Dr. Suzana Samson Nyanda kutoka Ndaki ya Sayansi za Jamii na Insia SUA akimuelezea Hayati Sokoine alivyokuwa kiongozi mchapakazi na mzalendo aliyefuatilia utekelezaji kwa vitendo. Katika Video |
0 Comments