Na: Calvin Gwabara
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo imeridhishwa na utekelezaji wa majukumu ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) hasa katika kuzalisha wataalamu wenye ubora kupitia Mafunzo kwa Vitendo pamoja na uongezaji thamani katika mazao ya kilimo na uzalishaji.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Prof. Kitila Mkumbo mara baada ya kufanya ziara kujionea kazi mbalimbali na miradi inayotekelezwa na SUA ambapo amesema wao kama wabunge wataendelea kuisisitiza Serikali na kuishauri kuongeza fedha za maendeleo na tafiti ili Chuo hicho kiweze kufanya kazi kubwa zaidi kwa maslahi mapana ya Taifa.
“Kwa kweli sote tunafahamu kuwa kazi kubwa za Chuo Kikuu ni tatu ambazo ni Kutoa Mafunzo, Kufanya Tafiti na kutoa Ushauri wa Kitaalamu lakini niwapongeze sana SUA kwa kujiongeza na kuongeza kazi nyingine muhimu ya kuongeza thamani kwenye uzalishaji hakika hili ni jambo la kuiga na tungeomba wizara ione jambo hili zuri lifikishwe na kwenye vyuo vingine” amesema Mhe. Prof. Mkumbo.
Aidha ameongeza kuwa kwa mujibu wa taarifa ya Chuo Kikuu cha Sokoine Cha Kilimo asilimia 95 ya fedha za utafiti zinatoka kwa wafadhili nje ya nchi ambao tafiti zinazofanyika ni kwa kuzingatia mahitaji na agenda za wafadhili hivyo ameahidi kupitia Kamati hiyo kuiomba Serikali kuongeza fedha za utafiti ili zifanyike tafiti ambazo zitajibu mahitaji ya Tanzania na vipaumbele vyake.
Kwa upande wake Mhe. Dkt. Thea Medard Ntara ambaye ni Mbunge upande wa Vyuo Vikuu na Taasisi ya Elimu ya Juu amesema SUA ni kati ya vyuo bora nchini na hakuna anayeweza kupinga hilo kutokana na matunda ya kazi zake lakini amekitaka Chuo hicho kuendeleza jitihada za kutangaza kazi za Chuo ili watanzania wengi zaidi wazifahamu na kuzitumia katika kusaidia jamii.
Pia ameomba uongozi wa Chuo na Wizara kuona namna ya kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha Kampasi ya Tunduru ili jamii ya mikoa hiyo iweze kufaidi matunda ya kazi za Chuo hicho kwa kuanzisha kozi mbalimbali za kilimo na kusaidia kutoa ushauri wa kitaalamu kupitia kituo hicho cha mafunzo.
Akitoa taarifa ya Chuo, Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Elimu kwa kuipatia SUA kiasi cha shilingi bilioni 73.6 kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) ambao unakwenda kuleta mageuzi na maboresho makubwa katika Chuo kwenye upande wa majengo, vifaa vya kufundishia, mafunzo kwa watumishi pamoja na kununua mitambo mbalimbali ya uzalishaji.
Prof. Chibunda amesema Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo ndio Chuo nguli katika masuala ya Misitu kwenye ukanda wote wa Afrika Mashariki na nchi zote zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC) ndio maana nchi zote kwenye ukanda huo zinaleta vijana wao kusoma katika Chuo hiki kutokana na ubora wake.
“Mhe. Mwenyekiti na wajumbe wa Kamati hiki Chuo chetu kina kauli mbiu kuwa SUA sio chuo cha maigizo wala eneo la kijana kuja kukulia hapa sisi tumejidhatiti kwa kuhakikisha tunazalisha wataalamu wazuri watakaoleta tija kwenye jamii na taifa letu.” alisisitiza Prof. Chibunda.
Makamu huyo wa Mkuu wa Chuo akijibu swali la Mbunge wa Morogoro Vijijini Mhe. Hamisi Shabani Taletale kuhusu mchango wa SUA katika kusaidia kilimo cha viungo kwenye Jimbo lake amesema tayari wameshakaa na Katibu Tawala wa mkoa kwa ajili ya suala hilo na Chuo kipo tayari kusaidia upatikanaji wa mbegu za kutosha kwa wakulima wa viungo Morogoro vijinini.
Akijibu baadhi ya hoja za Wabunge Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Kipanga, amepongeza kazi nzuri zinazofanywa na SUA na kuahidi kama Serikali kuendelea kushirikiana na Chuo katika kukiwezesha rasilimali fedha ili kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
Mhe. Kipanga amesema wamepokea maoni na mapendekezo yote yaliyotolewa na wabunge katika kuboresha utendaji wa kazi za Chuo huku akimuahidi Mhe.Thea Ntara kuwa Wizara imepanga kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha Kituo cha Mafunzo cha Ifinga kilicho chini ya SUA ili kuweze kufanya kazi vizuri na kusaidia jamii ya watu wa mikoa hiyo.
Kamati hiyo ya Bunge pamoja na mambo mengine imeridhia kwa pamoja kumpongeza Prof. Rudovic Kazwala kwa kuwa Mtafiti Bora Tanzania kutokana na kazi za tafiti zake kusomwa zaidi Duniani na kumuomba Makamu Mkuu wa Chuo kumfikishia salamu za pongezi kwa kazi yake nzuri.
Kamati hiyo ya Bunge ya Elimu,Utamaduni na Michezo imetembea miradi mbalimbali inayotekelezwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo ikiwemo Kituo cha Utafiti na Mafunzo cha Uchumi wa Bluu, Hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Wanyama, Jengo Mtambuka la Mafunzo pamoja na Kituo Atamizi cha Vijana.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda akizungumza mbele ya kamati hiyo mara baada ya kamatihiyo kutembea miradi inayotekelezwa na Chuo. |
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi an Teknolojia Prof. Carolyine Nombo akizungumza na kutoa ufafanuzi wa maoni na maswali mbalimbali ya Wabunge hao. |
Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Juma Kipanga (Mb) akitoa maelezo mbele ya kamati ya bunge kuhusu maoni na michango mbalimbali iliyotolewa na wabunge hao. |
Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Juma Kipanga (Mb) akizungumza na Waandishi wa habari akiwa kwenye kitengo cha Ufugaji viumbe maji (Blue Economy) |
Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Chakula na Teknolojia Dkt. Rashid Suleiman (Wa kwanza kulia) akiwaelezea wabunge namna ambavyo maabara ya Chakula ya Chuo Kikuu cha Sokoine inavyofanya kazi. |
Mhe. Dkt. Thea Medard Ntara ambaye ni Mbunge upande wa vyuo vikuu na Tasisi ya elimu ya juu akizungumza na wanafunzi wa kike wanaosoma Shahada ya Viumbe maji katika Chuo Kikuu cha Sokone cha Kilimo. |
Kamati ya kudumu ya Bunge ya Elimu,Utamaduni na Michezo akiwa kwenye ziara kutembea Hospitali ya Taifa ya Rufaa yaWanyama iliyo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo. |
0 Comments