SUAMEDIA

Sekretarieti ya Azimio la Nairobi waridhishwa na utekelezaji wa mradi wa EFLOWS nchini Tanzania.

 Na: Amina Hezron,Mbeya

Imeelezwa kuwa matokeo ya Utafiti wa Mradi wa Tathimini ya Maji kwa Mazingira (EFLOWS) unaotekelezwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) yanatarajiwa kwenda kutumika kama mfano kwenye nchi kumi za Afrika katika ukanda wa magharibi mwa Bahari ya Hindi ambazo zinakabiliwa na changamoto za uhifadhi kama ilivyo kwenye mto Mbarali.

Kiongozi wa Sekretarieti ya Azimio la Nairobi, Dixon Waruinge wakati akiongea na Wanajumuiya ya watumia maji Mbumtilu katika wilaya ya Wanging`ombe Mkoani Njombe

Hayo yameelezwa na kiongozi wa Sekretarieti ya Azimio la Nairobi, Dixon Waruinge wakati alipokuwa akifafanua kuhusu umuhimu wa Mradi wa EFLOWS pamoja na lengo ya ziara yao ya tathimini toka mradi huo kuanza kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Kanali Denis Filangali Mwila na maafisa wengine kutoka Ofisi ya Makamu wa Raisi Mazingira.

Amesema kuwa utaalamu wa kuhifadhi maji kwenye mito haupo kwenye nchi nyingi za Afrika ya Mashariki na hivyo ikaonekana uanzishwe mradi huo ambao utasaidia kuongeza elimu na ufahamu juu ya taaluma hiyo.

“kazi kubwa inayofanywa na watafiti hawa hapa Tanzania siyo kazi ya Tanzania peke yake japokuwa inafanyika Tanzania ni kazi ya nchi kumi, elimu bora tutakayoitoa hapa ni lazima tuieneze kwa nchi nyingine ili tukaseme kuwa inawezekana kwasababu watanzania wameweza na wametuonyesha njia na uzuri ni kuwa Prof. Japhet Kashaigili ni mmoja ya wale wanaoeneza elimu hiyo, hivyo tumpe nguvu hapa Tanzania elimu hiyo aipeleke nchi nyingine maana hata sasa anahusika katika kazi kama hiyo huko Madagasca”, alisema Waruinge.

Akieleza sababu za kuchagua mto huo Mtafiti Mkuu wa Mradi EFLOWS kutoka SUA Prof. Japhet Kashaigili amesema kuwa mto Mbarali ni mto ambao awali ulikuwa ukitiririsha maji mwaka mzima lakini miaka ya karibuni mto huo umeanza kukata maji hivyo kuna maswali ya kujiuliza ni nini kinapelekea hali hiyo.

“Hii hali imeleta changamoto ambayo tunajaribu kutafakari kwa sababu tunaiangalia katika upana mkumbwa kwamba serikali ipo katika jitihada kubwa ya uendelezaji wa miradi ya kimkakati kama nchi na moja ni Mradi wa Kufua Umeme wa Mwalimu Nyerere ambapo bila maji mradi huu hauwezi kuwa endelevu na mto Mbarali unachangia maji kwenye bwawa lile lakini sasa mto unakauka hasa eneo la chini”, alieleza Prof. Kashaigili.

Prof. Kashaigili amesema miaka michache iliyopita Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa Makamu wa Rais aliunda kamati ya kitaifa ya kuangalia changamoto hizo na yeye alikuwa ni mmoja wa wataalamu  walitoa mapendekezo na maazimio mengi ya mambo ya kufanya na hiki wanachofanya sasa ni sehemu ya kutekeleza mapendekezo yale.

Aidha ameongeza kuwa mradi huo ni wa mfano kwakuwa wana ainisha athari zitokanazo na shughuli za kibinadamu na jinsi ambavyo zinaathiri mtiririko wa maji kwenye mito lakini pia wanaangalia namna ya kupunguza athari hizo kwa kushirikiana na wadau wote walio kwenye maeneo hayo.

Amesema pamoja na utafiti wao, pia wameanzisha vitalu vya miche rafiki wa maji ambapo miche 45,000 imeoteshwa na zoezi la kupanda linaendelea kwenye vyanzo vya maji ambavyo vimeathirika na shughuli za kibinadamu pamoja na kingo za mito ndani ya mita 60 kwenye maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Wanging’ombe lakini pia kwenye Wilaya ya Mbarali ili kurudisha uoto wa asili.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Kanali Denis Filangali Mwila amepongeza kazi hiyo inayofanywa na watafiti hao kwa kushirikiana na Serikali katika kusaidia kupatikana kwa ushahidi wa kisayansi unatokana na tafiti ili kuweza kuyapa nguvu maamuzi yoyote yanayofanywa na  Serikali katika bonde hilo muhimu linalotegemewa na miradi ya kimkakati.

Aidha mkuu huyo wa Wilaya ya Mbarali amesema wao kama viongozi na Serikali wanatambua umuhimu wa Bonde hilo kama chanzo kikubwa cha maji kuelekea kwenye miradi mikubwa ya kufua umeme lakini pia wanatambua uhitaji wa maji kwa wananchi katika kufanya shughuli za kilimo lakini maamuzi yoyote yanayofanywa yazingatie maslahi mapana ya Taifa kiuchumi na sio watu wachache ambao wanaweza patiwa maeneo mengine ya kufanya kilimo na wakaendelea kuishi na kustawi.

“ Sisi kama Serikali ya wilaya tupo tayari kutoa ushirikiano wa hali na mali katika kuhakikisha matokeo ya utafiti huu yanapatikana na utaalamu wake unatumika katika kufanya maamuzi sahihi kuhusu bonde hili na mito yake na hapa ningependa kuomba wataalamu wetu mtoe ushauri vyema, mfano swala la watu kuondoka kwenye bonde lilikuwa wazi lakini baadae likatolewa tamko la kuwacha walime kwa mwaka mmoja ndio waondoke lakini mimi natamani tunapoamua kufanya maamuzi magumu tufanye maamuzi magumu kwa faida na maslahi mapana ya taifa letu”, alifafanua Mhe. Kanali Mwila.

Aidha amesema kauli hiyo inaweza kuleta athati kubwa zaidi kwenye eneo hilo kwani kwakuwa wanajua wameambiwa walime msimu mmoja ndio waondoke wanaweza kuongeza maeneo ya kilimo ili wavune zaidi kupata faida kubwa lakini matokeo yake  uharibifu ukawa mkubwa kwakuwa wanajua wanaondoka.

Mradi huu wa Utafiti unatekelewa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na kutekelezwa katika bonde la mto Rufiji ndani ya dakio la mto Mbarali kwa ushirikiano na Bodi ya Maji ya mto Rufiji, jumuiya za watumia maji, Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Wilaya ya Mbarali na Wanging`ombe na jamii, kwa ufadhili wa program ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa, UNEP na kutekelezwa kupitia Sekretarieti ya Azimio la Nairobi.


Mtafiti kutoka Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Bi. Rose Mtui akitoa salamu za NEMCH 

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali Mwl. Missana Kwangura akieleza mikakati ya Halmashauri yake katika kuunga Mkono juhudi za Mradi huo katika uhifadhi wa vyanzo vya maji na mito.

Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Kanali Denis Filangali Mwila akieleza msimamo wa Wilaya yake katika kuunga Mkono Jitihada za Watafiti na Serikali katika kitunza vyanzo vya maji.

Kiongozi wa Sekretarieti ya Azimio la Nairobi, Dixon Waruinge akiangalia sehemu ya miti rafiki wa maji iliyopandwa kwanye vyanzo vya maji.

Watafiti wa mradi wa EFLOWS, Maafisa kutoka Ofisi ya Makamu wa Riasi Mazingira, Maafisa kutoka  Sekretarieti ya Azimio la Nairobi, na Jumuiya ya watumia maji ya MBUMTILU wakijadiliana jambo wakati wakiangalia moja ya chanzo cha maji kilichoharibiwa na shughuli za binadamu na sasa kimepandwa miti rafiki wa maji kurudisha uoto wake wa asili.  

Mkurugenzi Msaidizi  wa Ofisi ya Makamu wa Raisi Mazingira Bw. Thomas Bwana kitoa salamu za Mkurugenzi ofisi ya makamu wa Raisi Mazingira wakati wa kikao cha pamoja na Jumuiya ya MBUMTILU.

Mtafiti Mkuu w Mradi wa EFLOWS kutoka SUA Prof. Japhet Kashaigili akitoa  neno kwa timu ya wataalamu hao mbele ya ya Wanajumuiya wa MBUMTILU kuhusu kazi ambazo mradi umezitekeleza na mafanikio yaliyofikiwa kwa kushirikiana na jumuiya hiyo ya MBUMTILU.

Post a Comment

0 Comments