SUAMEDIA

Wanawake na Wanafunzi watakiwa kuongeza ubunifu katika utekelezaji wa majukumu yao

Na. Vedasto George.

Imeelezwa  kuwa Wafanyakazi Wanawake katika  Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA wamekuwa wakichangia  kwa kiasi kikubwa katika kuhakikisha Chuo hicho kinafikia malengo yake ya utoaji wa huduma kwa jamii ikiwemo kushiriki katika kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia. 

Hayo yameelezwa na Prof. Yasinta Muzanila kutoka SUA wakati akifungua Semina ya siku moja kwa Wafanyakazi Wanawake na Wanafunzi wa Chuo hicho iliyolenga kuwajengea uelewa kuhusu Majukumu, Haki na Wajibu wa Mwanamke mahala pa kazi. 

Prof. Muzanila pia amewasisitiza Wanawake  na Wanafunzi kuhakikisha wanaongeza ubunifu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ili  kuongeza tija zaidi katika eneo lao la kazi.


“Tutanufaika sana na kupata uelewa mkubwa katika mada zitakazotolewa siku hii ya leo, wafanyakazi wanawake wanazo haki mbalimbali lakini tukumbuke kuwa hakuna haki isiyokuwa na wajibu hivyo kila Mfanyakazi anatakiwa  kutimiza wajibu wake tuwapo sehemu zetu za kazi”, amesema Prof. Muzanila.

Akisoma Risala kwa niaba ya Wanawake wafanyakazi wa SUA  Bi. Halima  Salum ambaye ni Katibu wa Kamati ya Wanawake RAAWU Tawi la SUA amesema mafunzo hayo yataongeza ufanisi katika utendaji kazi ikiwemo kutambua haki na wajibu  wao mahala pa kazi.

Kwa upande wake Dkt. Charles  Moses Lyimo ambaye ni Mratibu wa  Dawati la Jinsia Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA amesema SUA ni  miongozi mwa Taasisi zinazolinda na kupigania haki za kijinsia kwa pande zote ikiwemo haki ya mwanamke mahali pa kazi, umuhimu wao na  mazingira salama ili kuwawezesha na kufanya kazi kwa ufanisi.

Aidha Dkt. Lyimo ameongeza kuwa licha ya kuwepo kwa matukio ya ukatili wa kijinsia kwenye jamii, wazazi na walezi wanatakiwa kushikamana katika kutoa malezi bora kwa watoto ikiwemo kuwaambia watoto juu ya madhara  yatokanayo na matukio ya ukatili wa kijinsia.

Akitoa Mada kuhusu Majukumu ,Haki na Wajibu wa Wanawake mahala pa kazi Bi. Flora Maira ambaye ni Mshauri wa masuala ya Wanawake Mkoa wa Morogoro amesema  ni muda sasa kwa wanawake kujitambua na kupinga matukio ya ukatili ili kuweza kuwa na kizazi chenye tija ambacho kitaongeza uzalishaji  katika Taifa.

Naye Milvan Charles Mwenyekiti wa Kampeini ya Kupinga Ukatili wa Kijinsia Mkoa wa Morogoro amesema uwepo wa mila potofu na tamaduni zisizo za kitanzania kwenye jamii zimekuwa zikichangia kuwepo kwa ongezeko kubwa la matukio ya ukatili wa kijinsia.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Wanawake RAAWU Tawi la SUA Bi. Enessa Mlay ameishukuru Menejimenti ya SUA kwa kuwezesha Semina hiyo ambayo imeratibiwa na Chama hicho kwa kushirikiana na Dawati la Jinsia SUA pamoja na wadau wengine ambapo washiriki wote walipewa vyeti.

Semina ya Wafanyakazi  wanawake na Wanafuzi wa Chuo Kikuu Cha Sokoine cha Kilimo SUA imefanyika ikiwa ni siku chache zimepita tangu kuadhimishwa kwa kilele cha Siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimishwa kila ifikapo Machi 8 kila mwaka.










KATIKA VIDEO


Post a Comment

0 Comments