Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza imeahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA za kuzalisha miche mingi zaidi baada ya kununua miche ya matunda takribani 10,000 kwa lengo la kwenda kuinua kipato cha wananchi katika halmashauri hiyo lakini pia kutekeleza agizo la Serikali la upandaji miti kwa ajili ya kuhifadhi mazingira hasa vyanzo vya maji.
Amebainisha hayo Afisa Kilimo wa Halmashauri hiyo William Kaswahili wakati akizungumza na Kitengo cha Mawasiliano na Masoko alipotembelea Kitengo cha Bustani SUA kwaajili ya kununua miche ya matunda kwa lengo la kwenda kufungua fursa za ajira kwa wakazi wa Halmashauri ya wilaya ya Ukerewe.
Amesema kama Halmashauri wana wajibu wa kuhakikisha wananchi wao wanakuwa na uchumi wa uhakika kwa maana ya upatikanaji wa fedha hivyo wakaona ni bora kuanza kuimarisha uzalishaji wa matunda yenye ubora na SUA ndio suluhisho lao.
Bw. Kaswahili amesema kwa siku za nyuma wakulima wao walikuwa wanategemea kipato kutoka ziwani kwa maana ya Uvuvi lakini kwa siku za hivi karibuni uvuvi umekuwa ukisuasua hivyo Miche hiyo waliyoichukua itasaidia kutatua changamoto ya kutegemea chanzo kimoja cha mapato ambacho ni Ziwa vile vile Imani yao ni kuwa miche hiyo itafungua fursa mbalimbali ikiwemo viwanda.
“Matunda yatakapokuwa mengi, matunda Bora tunaamini watu kutoka sehemu mbalimbali watavutika kuja kuanzisha viwanda vidogo vidogo na vya Kati kwa ajili ya kusindika mazao yatokanayo na matunda, vilevile tunaenda kufungua fursa ya kipato cha Halmashauri kutoka kwenye ukusanyaji wa tozo za usafirishaji wa mazao yanayotoka ndani ya wilaya”,
amesema Bw. Kaswahili.
Aidha ameziomba Halmashauri nyingine ambazo zipo katika maeneo ambayo yapo katika Wilaya hiyo kwenda SUA kuchukua Miche ya Matunda kwa kuwa kuna Miche mingi na yenye ubora ambapo watapatiwa ushauri wa kitaalam juu ya utunzaji wa Miche mpaka ukuaji wake ili kwa pamoja kwenda kuifanya Kanda ya Ziwa kuwa sehemu yenye uhakika wa upatikanaji wa matunda.
Kwa upande wake Msimamizi wa Shamba la Mafunzo Kitengo cha Bustani na Mbogamboga SUA Bw. Roman Mfinanga amemuahidi Afisa Kilimo huyo wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kuwa miche ambayo wameipata imezalishwa kwa ubora na kuzingatia taratibu zote za uzalishaji wa Miche.
Bw. Mfinanga amesema Kitengo cha Bustani SUA wataenda kushirikiana nao bega kwa bega kwa maana ya kuhakikisha upandaji wa miche hiyo kwenye Halmashauri yao unafanyika kwa kufuata taratibu zote ikiwemo utunzaji hadi uvunaji lengo ni kuhakikisha wanapata kile walichokitarajia kutoka SUA.
0 Comments