SUAMEDIA

PASS yaishukuru SUA, Serikali na Denmark kwa kusaidia kituo Atamizi

 

Na Gladness Mphuru

Taasisi ya kusaidia sekta binafsi katika kilimo (PASS) ambayo inashirikiana na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kuendesha Kituo Atamizi imekishukuru chuo hicho, Serikali ya Kifalme ya Denmark na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuwaatamia na kutoa ujuzi kwa vijana ili kupunguza ukosefu wa ajira nchini kupitia Sekta ya Kilimo.

Mdhamini wa PASS Trust Prof. Sylvia Temu (kushoto) akizungumza na viongozi mbalimbali walipotembelea kituo Atamizi (Picha zote na Ayoub Mwigune)

Shukrani hizo zimetolewa Machi 28, 2023 na Mdhamini wa PASS Trust Prof. Sylvia Temu, wakati walipokitembelea kituo hicho kilichopo katika Kampasi Kuu ya Edward Moringe mkoani Morogoro.

Amesema kuwa wamefurahishwa na juhudi za vijana hao takribani 40 kwa kujituma na kuwekeza muda wao kwa mwaka mmoja na nusu katika shughuli za kilimo kwenye kituo hicho, na hiyo inaonyesha wana maono ya na malengo.

"Lengo letu kubwa la kuja kutembelea kituo hiki ni kuja kujionea kwa macho kinavyoendelea, kujifunza na kuona ni changamoto gani zilizopo ili kwa pamoja kwa kushirikiana na SUA tuweze kuona namna ya kuzitatua"

Ameongeza kuwa wameyaona baadhi ya mazao yanayolimwa na Vijana hao ambayo ni Pilipili hoho, Matango na Matikiti matamu pia lakini changamoto kubwa wanayokumbana nayo ni ukosefu wa maji ya kutosha kutokana na athari za ukame iliyo ikumba nchi mwaka huu.

Kwa upande wake Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Sanga kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo amesema SUA imeahidi kujenga vitalu nyumba katika kituo hicho Atamizi ili kuwasaidia vijana hao kufanya Kilimo Biashara kwa tija.

Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Sanga (wa pili kutoka kulia) akizungumza na waatamiwa (hawapo pichani)

Kwa upande wake Mkurugenzi wa fedha na Utawala wa PASS Doreen Mangesho amesema wanajivunia kuwa na kituo hicho kwani vijana hao wanafundishwa mambo mbalimbali kama vile fedha na masoko hivyo amewaomba wadau wawaunge mkono hususani sekta binafsi na mashirika ya fedha ili vijana hao wanapomaliza muda wao katika kituo hicho waweze kujiendeleza.

Kwa niaba ya vijana hao waatamiwa Bi. Merry Mota anaejishughulisha zao la Pilipili hoho za rangi amesema amepata faida kubwa kupitia zao hilo na amewashauri na kuwakaribisha vijana waliopo mitaani kujiingiza kwenye kilimo zinapotokea fursa kama hizo.

Pichani (chini) ni matukio mbalimbali katika ziara hiyo













Post a Comment

0 Comments