Na Winfrida Nicolaus
Mkuu wa Majeshi nchini Afrika Kusini Thalita Mxakato ambaye anashugulika na Masuala ya Ulinzi nchini humo amefanya ziara katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kampasi ya Solomon Mahlangu kama alama ya uhusiano wa kindugu kati ya Tanzania na Afrika Kusini vilevile kuona sehemu ambayo ilikuwa nyumbani wakati wakipambania ukombozi katika nchi yao.
Mkuu huyo wa Majeshi ambaye aliambatana na Maafisa wengine wa Jeshi kutoka Jeshi la Afrika Kusini pamoja na Tanzania amesema amefurahi kuona bado historia ya kituo imehifadhiwa hasa matumizi ya majina ambayo yanatumika katika vitengo mbalimbali hapo SUA.
Mxakato amesema imekuwa ni fursa ya kipekee kufika sehemu ambayo iliwahifadhi kipindi ambacho hawakuwa na uhakika wa kurudi nyumbani kwao Afrika Kusini wakiwa hai vilevile bado eneo hilo limeendelea kuwa ni kituo cha mafunzo hivyo ni ishara ya kuwa sehemu hiyo ni ya kipekee hususani katika historia ya kupigania uhuru.
“Eneo hili ni alama kubwa sana kwa nchi yetu kwa kuwa imezalisha vijana wengi sana wa Afrika Kusini na yeye akiwa mmoja wao ambao kwa sasa wanamchango mkubwa sana kwa nchi yao kutokana na kile walichopitia na kujifunza kutoka Solomon Mahlangu SUA’’, amesema Thalita Mxakato.
Kwa upande wake Kaimu Amidi wa Shule Kuu Dkt. Benedicto Msangya amesema wageni hao toka Afrika ya Kusini wamekuja SUA ili kutembelea maeneo ya kihistoria na kuweza kujikumbusha mahali ambapo palikuwa ni nyumbani kwa kuwa kuna baadhi yao waliishi hapo Mazimbu vilevile wametembelea pia Kiwanda cha Samani kilichowasaidia kujikimu kipindi walipokuwa wakiishi eneo hilo.
Ameongeza kuwa ujio wa Mkuu wa Majeshi wa Afrika Kusini umelenga katika kuimarisha mahusiano baina ya nchi mbili kati ya Tanzania na Afrika Kusini vilevile unafanya SUA kuwa sehemu ya kihistoria ambapo watu wengine kutoka sehemu mbalimbali wakiona na kusikia tukio hilo itawahamasisha kuweza kutembelea SUA hasa Solomon Mahlangu kwa kuwa eneo hilo limeshakuwa ni eneo la kihistoria.
0 Comments