Na.Vedasto George - Gairo
Serikali mkoani Morogoro imeliomba Jeshi la Polisi na vyombo
vingine vinavyo jishughulisha na makosa
ya ukatili wa kijinsia kutumia Teknolojia
katika kutatua kesi za makosa ya ukatili ili kuweza kukomesha vitendo hivyo
viovu ambavyo vimeendelea kurudisha nyuma maendeleo na ukuaji wa uchumi kwa Wanawake.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Judith Nguli wakati akimwakilisha
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwasa katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake
Duniani ambayo imefanyika kimkoa katika
Halmashauri ya Wilaya ya Gairo.
Pia Mkuu huyo wa Wilaya amewataka Wanawake mkoani humo kuendelea kuwa wabunifu katika utekelezaji wa majukumu
yao na kwenda na kasi ya mabadiliko ya Teknolojia ili kuweza kujiendeleza
katika Sekta mbalimbali ikiwemo kukuza pato
la familia.
Aidha amesema kutokurejeshwa kwa mikopo ya asilimia kumi inayotolewa
na Serikali kupitia Halmshauri kuwa ni changamoto inayokwamisha ukuaji wa
uchumi kwa Wanawake na kusababisha wanawake walio wengi kuendelea kuwa tegemezi
jambo ambalo limepitwa na wakati katika zama hizi ambazo mabadiliko ya
tekinoloja yameendelea kuwa makubwa.
Awali akisoma risala kwa niaba ya Wanawake wa mkoa wa
Morogogo, Afisa Maendeleo ya Jamii mkoa wa Morogoro Bi. Tumaini Wapalila amesema
ili kufikia malengo yaTaifa ya kufikia katika uchumi imara katika viwanda ni
lazima wanawake wawezeshwe kwa kupewa elimu ya uendeshaji wa viwanda .
Akizungumzia changamoto zinazo wakabili wanawake kwa sasa Bi.
Tumaini amezitaja kuwa ni upatikanaji wa masoko katika bidhaa zinazozalishwa na
wajasiliamali ambapo ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuwasaidia masoko
ya bidhaa ikiwemo urasimishaji wa bidhaa ili ziweze kushindana katika soko la
kimataifa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Gairo Jabiri Omary Makame amesema Serikali
kwa kutambua mchango mkubwa unaotolewa na wanawake katika kukuza uchumi kupitia
halmashauri, imeendelea kutoa mikopo ambayo
inawawezesha wanawake kuweza kujiajiri.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Gairo Rael Nyangasi amewasistiza wazazi
kushirikiana katika kutoa malezi bora kwa Watoto kwa sababu sasa hivi dunia
inakabiliwa na changamoto kubwa ya matukio ya ukatili wa kijinsia.
Naye Mbunge wa Viti maalumu Jimbo la Morogoro Mh. Christina
Ishengoma amesema Wanawake wanatakiwa kutumia fursa ya mabadiliko ya Teknolojia
katika kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia ambavyo vinaendelea kushamiri
katika maeneo mbalimbali ya nchi.
“Wanawake tutumie Teknolojia
kupinga ukatili wa kijinsia tukifanya hivyo tunaweza kukomesha matendo haya
maovu na tuwe wa kwanza kutoa taarifa pale
tunapo yaona matukio haya ya kinyama ambayo wanafanyiwa Watoto wetu lakini kwa
akina mama na walemavu pia”, amesema
Mbunge huyo.
Aidha Mwenyekiti wa Kamati ya Wanawake kupitia Chama cha
Wafanyakazi RAAWU Tawi la SUA Bi. Enessa Mlay ameishukuru Menejimenti ya Chuo
Kikuu Cha Sokoine cha Kilimo SUA kwa kuwawezesha Wanawake wa Chuo hicho kuweza
kushirikiana na wanawake wengine wa mkoa wa Morogoro katika Maadhimisho hayo.
0 Comments