Na: Winfrida Nicolaus
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
(SUA) kimetoa vifaa vya TEHAMA vyenye thamani ya Shilingi Milioni 42.3 kwenye
Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu jijini Dodoma ili kuhakikisha
inaiunga mkono Serikali katika juhudi zake za kupambana na maafa nchini.
Prof. Karimuribo (aliyevaa kaunda suti nyeusi) akikabidhi vifaa vya TEHAMA kwa Naibu Mkurugenzi wa Maafa, Bwana Charles Msangi (mwenye tai)
Makabidhiano hayo yamefanyika
February 13, 2023 na Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji wa
Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Esron Karimuribo na Naibu Mkurugenzi wa Maafa, Ofisi
ya Waziri Mkuu Bw. Charles Msangi jijini Dodoma.
Amesema vifaa vilivyokabidhiwa ni
pamoja na Kitunza Kumbukumbu yaani ‘Server’, kifaa cha kupokea na kupiga simu ‘Call
Centre’ na Kompyuta nane za mezani kwa ajili ya kuimarisha Mfumo wa Mawasiliano
ya Kidigitali wakati wa maafa, hasa yale yatokanayo na milipuko ya magonjwa na
matukio mengine yanayoweza kudhuru afya ya Binadamu, Wanyama na, Mazingira.
Awali
wakati akikabidhi vifaa hivyo, Profesa Karimuribo amesema kuwa tangu mwaka 2021
ambapo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kupitia taasisi yake ya SACIDS
Foundation for One Health kimekuwa kikishirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu,
Idara ya Menejimenti ya Maafa -Kitengo cha Uratibu wa Afya Moja katika kuunda
Jukwaa Shirikishi la Mawasiliano ya Kidijitali.
“Lengo kuu
la uundwaji wa jukwaa hilo Shirikishi ni kuimarisha uwezo wa kitaifa wa kubaini
na kushirikisha kwa wakati wadau husika kudhibiti matukio na viashiria vya
milipuko ya magonjwa na matukio mengine yanayoweza kudhuru Afya ya Binadamu,
Wanyama na Mazingira”, amesema Prof. Esron Karimuribo
Kwa
upande wake Naibu Mkurugenzi wa Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Charles Msangi
wakati akipokea vifaa hivyo kwa niaba ya Serikali amekishukuru SUA kwa msaada
walioutoa ambao utawezesha kukabiliana na maafa kwa kutumia teknolojia ya
kisasa.
Ameongeza kuwa watavifanyia majaribio vifaa hivyo kwa muda wa miezi miwili na baadaye mfumo utazinduliwa rasmi na Serikali kwa kushirikisha umma wa Watanzania katika kupambana na maafa
0 Comments