SUAMEDIA

SUA kukabidhi rasmi Nyumba za Mapumziko kwa Serikali za Mitaa


Na Gladness Mphuru


Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimekabidhi rasmi Nyumba za Mapumziko tatu kwa Serikali za Mitaa, ili zitumike kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wa maeneo ya Matombo, Nyachiro, Malolo na Taifa kwa ujumla.

Prof. Raphael Chibunda (aliyekaa kushoto ) akitia saini ya makabidhiano rasmi katika  kukabidhi Nyumba tatu kwa Serikali za Mitaa, ili zitumike kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.

Makabidhiano hayo yamefanyika katika Kampasi Kuu ya Edward Moringe mkoani Morogoro, yakiongozwa na Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda na kushuhudiwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Prof. Riziki Shemdoe pamoja na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Bw. Mussa Ali Musa.

Aidha katika tukio hilo Prof. Chibunda amesema nyumba hizo zimeanza kutolewa tangu mwaka 2022, ambapo kabla ya hapo  Menejimenti ilifanya operesheni ya kukagua nyumba zake zote na kuonelea kuna nyumba ambazo hazitumiki stahiki ndipo ikaamua nyumba hizo zikabidhiwe kwa Mamlaka za Vijiji  katika maeneo tofauti.

Prof. Chibunda amebainisha kuwa uamuzi huo uliridhiwa kwa kuwa Chuo hakitumii nyumba hizo kwa sasa na kupelekea Baraza la Chuo kuridhia mapendekezo kutoka kwa Menejimenti juu ya kugawa nyumba zake kwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa kupitia Ofisi ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na kuvitaja nyumba hizo za mapumziko kuwa ni Kibogwa iliyopo Morogoro vijijini, Nyachiro iliyopo Mvomero na Malolo kiliyopo wilayani Kilosa.

Aidha, ameishukuru Serikali ya Mkoa wa Morogoro inayoongozwa na Mama Fatuma Mwasa na Katibu Tawala Musa Ally Musa pamoja na viongozi wa vijiji vya Matombo, Nyachiro na Malolo kwa ushirikiano wao na kuwashauri viongozi hao kuzifanyia nyumba hizo ukarabati.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Prof. Riziki Shemdoe akizungumza wakati wa makabidhiano ya Nyumba za Mapunziko SUA.

Kwa Upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Prof. Riziki Shemdoe ameishukuru Menejimenti na Baraza la Chuo SUA kwa uamuzi huo ili Serikali za vijiji ziweze kuzitumia kwa manufaa ya wanachi wa vijiji hivyo.

“Nimeona jitihada ambazo zimefanywa na SUA kwa kutafuta ardhi kwenye maeneo ya vijiji vyetu hivi vitatu na ninafahamu maeneo mengine ambayo mmefanya kazi na kupata ardhi naomba niwahakikishie kwamba jitihada zenu hazitapotea zitaendelea kutunzwa na kuzitumia vizuri” Amesema Prof. Shemdoe.

Aidha amewaasa viongozi hao wa vijiji watoe kipaumbele kwa kuwapa majengo hayo ya kuishi watu wanaotoka Sekta ya Elimu na Afya ili waweze kuwasaidia kupata huduma bora.

Akitoa neno la shukrani Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mussa Ali Musa ameishukuru Menejimenti ya SUA na kuahidi kuhakikisha maeneo hayo yanatumika vyema kwa manufaa ya wananchi.







Post a Comment

0 Comments