SUAMEDIA

SUA yatoa vifaa vya TEHAMA kwa Serikali

 Na: Winfrida Nicolaus

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimetoa vifaa vya TEHAMA vyenye thamani ya Shilingi Milioni 42.3 kwenye Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu jijini Dodoma ili kuhakikisha inaiunga mkono Serikali katika juhudi zake za kupambana na maafa nchini.


Prof. Karimuribo (aliyevaa kaunda suti nyeusi) akikabidhi vifaa vya TEHAMA kwa Naibu Mkurugenzi wa Maafa, Bwana Charles Msangi (mwenye tai)

Makabidhiano hayo yamefanyika February 13, 2023 na Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Esron Karimuribo na  Naibu Mkurugenzi wa Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Charles Msangi jijini Dodoma.

Amesema vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na Kitunza Kumbukumbu yaani ‘Server’, kifaa cha kupokea na kupiga simu ‘Call Centre’ na Kompyuta nane za mezani kwa ajili ya kuimarisha Mfumo wa Mawasiliano ya Kidigitali wakati wa maafa, hasa yale yatokanayo na milipuko ya magonjwa na matukio mengine yanayoweza kudhuru afya ya Binadamu, Wanyama na, Mazingira.

Awali wakati akikabidhi vifaa hivyo, Profesa Karimuribo amesema kuwa tangu mwaka 2021 ambapo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kupitia taasisi yake ya SACIDS Foundation for One Health kimekuwa kikishirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Menejimenti ya Maafa -Kitengo cha Uratibu wa Afya Moja katika kuunda Jukwaa Shirikishi la Mawasiliano ya Kidijitali.

Lengo kuu la uundwaji wa jukwaa hilo Shirikishi ni kuimarisha uwezo wa kitaifa wa kubaini na kushirikisha kwa wakati wadau husika kudhibiti matukio na viashiria vya milipuko ya magonjwa na matukio mengine yanayoweza kudhuru Afya ya Binadamu, Wanyama na Mazingira”, amesema Prof. Esron Karimuribo

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Charles Msangi wakati akipokea vifaa hivyo kwa niaba ya Serikali amekishukuru SUA kwa msaada walioutoa ambao utawezesha kukabiliana na maafa kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

Ameongeza kuwa watavifanyia majaribio vifaa hivyo kwa muda wa miezi miwili na baadaye mfumo utazinduliwa rasmi na Serikali kwa kushirikisha umma wa Watanzania katika kupambana na maafa 


Post a Comment

0 Comments