SUAMEDIA

SUA yaendelea kujenga uelewa wa kijinsia kwa wafanyakazi na wanafunzi chuoni

 Na Gladness Mphuru

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimetengewa fedha kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni 32 sawa na Shilingi Bilioni 73 kupitia Mradi wa 'Higher Education for Economic Transformation' (HEET) ambapo Dola Milioni 24 zitatumika kwa Kampasi za Morogoro na Milioni 8 Kampasi ya Katavi katika kuboresha Miundombinu na kuboresha usawa wa Kijinsia kwa Mageuzi ya Kiuchumi Nchini.


Rasi wa Ndaki ya Sayansi za Jamii na Insia Prof. Kabote akizungumza katika warsha ya siku moja ya kujengea uwezo wa kijinsia wafanyakazi na wanataaluma SUA (Picha zote na Winfrida Mwakalobo)

Hayo yamebainika February 2, 2023 katika Kampasi Kuu ya Edward Moringe Mkoani Morogoro katika warsha ya siku moja ya kuwajengea uwezo wa Kijinsia washiriki ambao ni wafanyakazi wanataaluma na wasio wanataaluma pamoja na wanafunzi, ambayo imefunguliwa na Rasi wa Ndaki ya Sayansi za Jamii na Insia Prof. Samwel Kabote.

Akizungumza kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda, Rasi wa Ndaki ya Sayansi za Jamii na Insia Prof. Kabote amesema lengo la warsha hiyo ni kueleza dhana ya kijinsia, sera husika na mifumo ya kisheria katika masuala yanayohusiana na jinsia, kuunganisha mitazamo ya kijinsia katika vikao vya Sera za Chuo Kikuu, kuchukua jukumu katika kuandaa na kutumia sera na miongozo kwa lengo la kuboresha usawa wa kijinsia chuoni

"Nashukuru Dawati la Jinsia kwa kuandaa warsha hii muhimu kwa sababu mbali na mambo mengine jinsia ni moja kati ya masuala mtambuka kwa maendeleo na sisi kama SUA tunapaswa kuzingatia suala hili kwa uzito " amesema Prof. Kabote


Baadhi ya wanafunzi na wafanyakazi wakifuatilia mafunzo

Amesema Taasisi ya SUA ina mtazamo chanya wa kijinsia katika sera na programu zake, hivyo lazima waweze kuwa na dawati la jinsia ambalo litaweza kudhibiti masuala yote ya kijinsia, na tayari upo mchakato wa kuanzisha madawati ya jinsia kwa msaada wa Prof. Jeckonia ambae ni mmoja wa wataalamu wa masuala hayo.

Kwa Upande wake Kiongozi katika Mradi huo Kitengo cha Masuala ya Jinsia Prof. John Jeckonia amesema katika warsha hiyo muitikio kwa washiriki ni mzuri ambao idadi yao ni 65, ambapo wameweza kujadiliana na kubadilishana uzoefu wa masuala ya kijinsia, dhana za jinsia pamoja na umuhimu wa ujumuishwaji wa maswala ya Jinsia katika shughuli za chuo na mradi.


Kiongozi katika Mradi huo Kitengo cha Masuala ya Jinsia Prof. John Jeckonia akizungumza katika mafunzo hayo

"Tumepata timu nzuri ambayo itaendelea kufanya kazi katika kuingiza masuala ya Jinsia katika shughuli za kila siku kwa maana ya kufundisha, kufanya utafiti na katika shughuli zote cha Chuo" amesema Prof. Jeckonia

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa Warsha hiyo Afisa Utumishi Mwandamizi Bi. Hilda Chigudulu, ameushukuru uongozi wa Mradi wa HEET kupitia Dawati la Jinsia kwa kuandaa mafunzo hayo ya muhimu ambayo yatawasaidia kutimiza majukumu yao kwa viwango ambavyo vyuo vingine haviwezi kufikia na pia ameahidi utayari katika jambo hilo.

Post a Comment

0 Comments