Na Winfrida Nicolaus
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo amekipongeza Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa utekelezaji wa Miradi kwa vitendo na kuwataka
kuanzisha mfumo mzuri utakaowezesha kupata vijana ambao hawafikirii kuajiriwa
bali kujiajiri ili waajiri wengine kwa kuwa ndiyo njia pekee ya kulifanya Taifa
kufikia malengo yake ya kumkwamua mwananchi wa kawaida ambaye maisha yake
yanategemea Kilimo.
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo akizungumza na wafanyakazi na wanafunzi wa SUA (hawapo pichani) wakati wa ziara yake kujionea Miradi ya Maendeleo chuoni hapo (Picha zote na Gerald Lwomile)
Chongolo amesema hayo Februari 5, 2023 wakati alipotembelea Miradi ya
Maendeleo inayotekelezwa Chuoni hapo na kuzungumza na Wafanyakazi pamoja na
Wanafunzi katika ukumbi wa ‘Multipurpose’ Kampasi ya Edward Moringe Sokoine mkoani
Morogoro.
Chongolo amesema lazima kuwepo na lengo
la kuzalisha watu ambao wakiondoka
wataenda kuwa wawakilishi wazuri kwa maana
ya kutengeneza matokeo zaidi katika eneo lao la Taaluma hivyo nchi inahitaji kuwa na taaluma zinazoipeleka kwenye
uzalishaji wa moja kwa moja kwa kiwango cha juu na SUA ikiwa katika njia hiyo ya uzalishaji nchi itakuwa
na chakula cha kutosha kuliko sehemu nyingine Afrika na duniani kwa ujumla.
Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Raphael Chibunda (aliyeshika kipaza sauti) akitoa maeelezo kwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo wakati wa ziara chuoni hapo
Aidha amesema asilimia 80 ya Watanzania ni Wakulima na kutokana na hali hiyo
wanakuwa wadau wakubwa wa SUA kwa asilimia 100, mdau huyo anatakiwa kuwa na
uelewa wa kutosha juu ya kile anachokifanya na nchi hii inawaangalia wasomi
hususani katika kumtoa mkulima kutoka kwenye kulima kawaida na kwa ajili ya
tumbo kwenda kulima kibiashara kwa maendeleo yake binafsi na Taifa kwa
ujumla.
‘‘Mimi nimebahatika kuwa nakuja sana SUA kufuata miche ya Miti kwa sababu maisha yangu ni Kilimo, niwe mkweli nimeona mabadiliko makubwa
sana na ya kweli ambayo yanahitaji utashi tuliopewa na Mwenyezi Mungu kusogeza
kijiti ili mambo yaende nje na kutokea kuwa makubwa na naamini kupitia utaalamu
nilioendelea kujifunza SUA mabadiliko
yatakuwa makubwa sana na kwenda kunufaika zaidi kwa kile ninachokiamini”,
amesema Daniel Chongolo
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo (wa tatu kutoka kulia) akisikiliza maelezo ya uzalishaji wa mazao ya mbogamboga katika Atamizi iliyopo SUA ( wa nne kutoka kushoto) ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Bibi. Fatma Mwasa
Kwa upande wake Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha
Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda ameishukuru Serikali inayoongozwa
na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukipatia Chuo kiasi cha shilingi Bilioni
73.6 sawa na Dola za Kimarekani Milioni 32.6 kupitia Mradi wa 'Higher Education
for Economic Transformation' (HEET) ambapo wameahidi kwenda kutumia fedha hizo kujenga
na kupanua miundombinu mipya katika Kampasi zao za mafunzo yaani Edward
Moringe, Solomoni Mahlangu na Mizengo Pinda.
Aidha, amesema Chuo kitaenda kuboresha mitaala yake
ili iweze kuakisi mahitaji ya Soko la Ajira kwa kununua Vifaa vya kisasa vya
Mafunzo pamoja na kupeleka wafanyakazi katika Mafunzo hivyo kupitia Mradi huo
wataenda kutekeleza kwa nguvu zao zote na uadilifu mkubwa kwa kuhakikisha
waliyoyapanga yanaenda kutokea kweli
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo alikuwa na ziara
ya siku tisa (9) Mkoani Morogoro ambapo ilianza Januari 27 , 2023 na kuhitimishwa
Februari 5, 2023 siku ya Kilele cha Maadhimisho ya Miaka 46 ya Chama cha
Mapinduzi (CCM) tangu kuanzishwa kwake mwaka 1977
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo (aliyevaa kofia) akipokea zawadi ya mboga, viungo na matunda kutoka kwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda (wa pili kulia)
0 Comments